Mbunge wa Jimbo la Nyasa Mheshimiwa Stella Manyanya kushoto,akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini Mhandisi Clement Kivegilo kuhusiana na mikakati ya kumaliza kero ya maji kwa wakazi wa jimbo hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegilo kulia, akimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Nyasa mkoani Ruvuma Mheshimiwa Stella Manyanya wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji inayotekelezwa katika vijiji mbalimbali mkoani Ruvuma.
Tenki la kuhifadhi maji linaloendelea kujengwa kwenye mradi wa maji katika kijiji cha Mwerampya Jimbo la Nyasa kama linavyoonekana.
…………………….
Na Muhidin Amri,
Nyasa
MKURUGENZI Mkuu wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)Mhandisi Clement Kivegilo amesema,kuna haja ya Serikali kuanza mchakato wa kutumia maji ya ziwa Nyasa ili kumaliza shida ya maji kwa wananchi,badala ya kuendelea kutegemea vyanzo vya maji ambavyo sio vya uhakika.
Kivegilo amesema hayo kwa nyakati tofauti,wakati akikagua ujenzi wa miradi mikubwa ya maji katika kata ya Liuli na Lituhi Halmashauri ya wilaya Nyasa mkoani Ruvuma inayojengwa kwa gharama ya Sh.bilioni 11.3
Kivegilo alisema,hakuna sababu ya wilaya ya Nyasa kuwa na tatizo la maji kwa wananchi wake,kwani kuna vyanzo vingi na uhakika ikiwamo ziwa Nyasa lenye uwezo wa kuhudumia wilaya yote ya Nyasa.
“unaposikia watu wana shida ya maji na wanaishi kando ya ziwa nyasa haiingii akilini hata kidogo,wakati umefika sasa kwa serikali kuanza mchakato wa kutumia maji ya ziwa Nyasa badala ya kuendelea kutegemea vyanzo vingine ambavyo havina uhakika sana”alisema Kivegilo.
Miradi hiyo ni mradi wa maji Liuli unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 5 na mradi wa maji wa Mwerampya kata ya Lituhi unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh.bilioni 6.5.
Amemwagiza Mkandarasi kampuni ya Emirate Co Ltd anayejenga miradi hiyo,kuhakikisha anakamilisha kazi kabla ya muda aliopewa ili wananchi waanze kupata huduma ya maji katika maeneo yao.
Amamtaka kukamilisha ujenzi wa vituo vya kuchotea maji,ili huduma ya maji ianze kufika kwa wananchi huku kazi nyingine zikiendelea kufanyika kwani hakuna sababu ya wananchi kutopata maji kama mradi umefikia asilimia zaidi ya 65 ya utekelezaji wake.
Kwa mujibu wa Kivegilo ni kwamba,miradi yote ni ya mserereko hivyo hakuna changamoto kubwa katika utekelezaji wake, kwa hiyo ni vyema mkandarasi akaongeza nguvu ili ikamilike haraka na kuanza kutoa huduma na wananchi wa vijiji hivyo wafurahie matunda ya Serikali yao ya awamu ya sita.
Alisema kwa sasa kazi zilizobaki siyo kubwa, hivyo mkandarasi ana uwezo wa kukamilisha ujenzi wa miradi hiyo kabla ya muda aliopewa kwa sababu kampuni hiyo ina uwezo mkubwa katika kujenga miradi ya maji hapa nchini.
Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa wilaya ya Nyasa Jeremiha Maduhu alisema,miradi hiyo yote inatarajiwa kukamilika mwezi Aprili 2023 na itawanufaisha zaidi ya wakazi 28,000.
Naye Mbunge wa jimbo la Nyasa Stella Manyanya,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kutoa fedha zaidi ya Sh.bilioni 11 ambazo zinakwenda kutumika kujenga miradi miwili mikubwa ambayo itamaliza tatizo la muda mrefu la huduma ya maji safi na salama.
Hata hivyo,ameiomba wizara ya maji kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira(Ruwasa)kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga miradi mingine ya maji katika vijiji vyenye changamoto kubwa ya huduma hiyo.
Mkazi wa Nyasa Said Rashid alisema,kwa muda baadhi ya maeneo ya Jimbo la Nyasa wanakabiliwa na changamoto kubwa ya maji katika maeneo yao.
Alisema,kujengwa kwa miradi hiyo kutapunguza kero hiyo hasa kwa wanawake na watoto wanaolazimika kuamka usiku wa manane kwenda kutafuta maji kwevye vyanzo vichache vilivyopo.