Meneja wa Ruwasa wilaya ya Njombe Mhandisi Elikalia Malisa kushoto,akimuonesha Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo mchoro wa ujenzi wa mradi wa maji unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh.milioni 800 katika kijiji cha Nyombo wilayani humo.
Meneja wa Ruwasa mkoa wa Njombe Mhandisi Sadick Chakka kulia,akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo aliyetembelea mradi wa maji Nyombo unaotekelezwa kwa gharama ya Sh.milioni 893,730,555 fedha za mfuko wa maji(NWF).
Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo akikagua miundombinu katika ujenzi wa mradi wa maji Nyombo wilayani Njombe,kushoto kwake Meneja wa Ruwasa mkoa wa Njombe Sadick Chakka.
Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo akipanda juu kukagua ubora wa ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji katika mradi wa maji Nyombo wilayani Njombe,anayeangalia chini Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu wa Ruwasa Bwai Biseko.
Tenki la maji linalojengwa katika mradi wa maji kijiji cha Nyombo wilayani Njombe likiwa katika hatua ya mwisho kukamilika.
Picha zote na Muhidin Amri
…………………………….
Na Muhidin Amri,
Njombe
WAKALA wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Njombe mkoa wa Njombe,umeanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji utakaowanufaisha wakazi 4,144 wa kijiji cha Nyombo wilayani humo.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Njombe Elikalia Malisema alisema,lengo la kujenga mradi huo ni kuwapunguzia wananchi wa kijiji cha Nyombo adha ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji mbali na makazi yao.
Alisema,mradi wa maji Nyombo unafadhiliwa na serikali ya Tanzania kwa gharama ya Sh.milioni 893,730,555 kupitia mfuko wa maji(NWF) ambapo muda wa utekelezaji wake ni muda wa miezi sita.
Alisema, kati ya fedha hizo Serikali imeshatoa Sh.milioni 134,059,583.37 ambazo zimetumika kulipwa mkandarasi na kiasi cha fedha kinachodaiwa ili kukamilisha ujenzi wa mradi ni Sh.milioni.
Malisa alisema, kazi zilizopangwa kutekelezwa katika mradi huo ni ujenzi wa chanzo,tenki dogo la juu,kulaza bomba kuu umbali wa km 11,kulaza mabomba ya kusambaza maji km 19.
Alitaja katika nyingine zilizopangwa kutekelezwa ni ujenzi wa vituo 36 vya kuchotea maji,kujenga nyumba ya pumpu,nyumba ya mlinzi na ujenzi wa njia ya meme kwenda kwenye chanzo.
Alisema,hadi sasa kazi zilizofanyika hadi sasa ni ujenzi wa mtego(chanzo) ambao umefikia asilimia 97,ujenzi wa tenki la juu,ulazaji wa bomba kuu km 1.3,kulaza bomba za kusambaza maji,ujenzi wa vituo vya kuchotea maji,nyumba ya pumpu,nyumba ya mlinzi na njia ya umeme ambapo utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 78.
Kwa mujibu wa Malisa,changamoto kubwa katika utekelezaji wa mradi ni kuanza kipindi cha masika hivyo kusababisha kazi ya upelekaji wa vifaa eneo la kazi kuwa ngumu na kasi ya ujenzi kuwa ndogo.
Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo amempongeza Meneja wa Ruwasa mkoa wa Njombe Sadick Chakka na meneja wa wilaya ya Njombe Elikalia Malisa na wafanyakazi walio chini yao kwa kazi nzuri katika kutekeleza na kusimamia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji.
Alisema,mkoa huo ni kati ya mikoa inayofanya vizuri kwenye ujenzi wa miradi ya maji na kuwashukuru wakandarasi wote wanaoendelea kujenga miradi hiyo kutokana na uzalendo na uaminifu wao kwa Serikali ya awamu ya sita kwani wakati mwingine wanalazimika kutumia fedha zao ili kukamilisha kazi.
Aliongeza kuwa,katika awamu zilizopita wakandarasi wengi walikuwa wanafukuzwa site(eneo la mradi) kutokana na utamaduni uliozoeleka wa kutumia fedha nyingi kuliko kazi zilizofanyika.
Kivegalo alieleza, katika awamu ya sita kazi kubwa inayofanyika ni kurejesha nidhamu ya matumizi ya fedha kwenye ujenzi wa miradi ya maji hapa nchini ili kuwaondolea wananchi kero kubwa ya upatikanaji wa huduma ya maji.
Aidha alisema,Ruwasa itahakikisha inawalipa wakandarasi wote wanaodai fedha za gharama za ujenzi wa miradi ya maji na kuwaomba kutanguliza uzalendo kwenye kazi zao badala ya kutanguliza maslahi binafsi.
Kivegalo ambaye yuko kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji katika mikoa ya nyanda za juu ya Ruvuma,Njombe na Iringa alisema, mpango wa Serikali kupitia Ruwasa ni kuhakikisha inaboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 95 kwa upande wa mijini na asilimia kwa vijijini.
Amemtaka Mkandarasi anayejenga mradi huo wa Nyombo kampuni ya Buldtech Engineering Co Ltd, kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi ili ifikapo mwezi Disemba wananchi wa kijiji hicho waanze kupata huduma ya maji safi na salama.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Nyombo Ezekia Mligula,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa mapenzi makubwa ya kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza mradi huo wa maji ambao unakwenda kumaliza kero kubwa ya maji.
Alisema,wananchi wa kijiji hicho wameupokea mradi huo kwa mikono miwili na sasa wana hamu kubwa ya kuona wanapata maji ya bomba katika maeneo yao.