***********************
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Nov 25
SERIKALI Mkoani Pwani, imeagiza wavunaji holela wa mazao ya misitu wanaovuna bila kufuata sheria kwenye hifadhi za Misitu na vyanzo vya maji waondoke mara moja katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Kufuatia hatua hiyo, imeweka msimamo kuanzia sasa inaendelea na operesheni ya usiku na mchana kuwaondoa wanaofanya shughuli za uvunaji wa mazao ya misitu.
Mkuu wa mkoa wa Pwani , Abubakari Kunenge akiwa pamoja na kamati ya usalama ya mkoa, viongozi wa Wakala wa huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki na wilaya ya Kibaha, alitoa tamko na maagizo hayo kwa waandishi wa habari Mkoani Pwani.
Alielezea kwamba, yeyote atakaekaidi agizo hilo atachukuliwa hatua za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine.
Alielezea kwamba, wafanyabiashara wa mkaa,wanaokata miti,kuni na fito ,muenendo huu haukubariki hata kidogo.
Aidha Kunenge aliwaasa wananchi kushiriki kikamilifu katika kuhifadhi vyanzo vya maji.
Mkuu huyo wa mkoa ,aliwataka viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya chini pamoja na wakuu wa wilaya wasimamie utekelezaji wa maagizo hayo pamoja na vibali vya uvunaji wa mazao ya misitu.
“Kuna uvunaji holela na misitu kwenye Maeneo ya vijiji, vyanzo maji, Misitu ya hifadhi kinyume cha sheria, kwasababu tunafahamu misitu hii ni maliasili ya Taifa na inavunwa na kutunzwa kisheria”
“Uvunaji ni mkubwa na tunashuhudia athari iliyopo sasa katika upatikanaji wa maji , wananchi waanze kuona umuhimu wa matumizi ya nishati mbadala ,Kwani uharibifu upo kwa kiwango kikubwa ,Tushirikiane kuendelea kupunguza tatizo hilo “alisisitiza Kunenge.
Wakati huo huo ,Kunenge alikemea mifugo holela na kusema mkoa umeanza kutambua na kutenga maeneo kwa ajili ya kuwapa wafugaji kuhifadhi mifugo yao.
Aliwataka wafugaji kuanza kufuga kwa tija ,kwa kubaki na mifugo michache wanayoweza kuimudu.
“Mifugo isidhurure ,sisi Kama mkoa kwa hatua ya Sasa tunatenga maeneo ya wafugaji ,wajue ardhi haiongezeki , wafugaji lazima wavune mifugo ili kubaki na mifugo michache yenye tija”