******************
Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dar es Salaam
Picha ya Mwl. Julius Nyerere na Oliver Tambo zimechorwa katika Ofisi ya Ukombozi wa Afrika jijini Dar es salaam ili kuweka sawa kumbukumbu ya historia ya ukombozi wa Afrika Kusini hatua inayosaidia kuenzi kazi zao walizofanya katika kuleta uhuru wa nchi hiyo.
Naibu katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema hayo Novemba 25 jijini Dar salaam wakati wa uzinduzi wa picha maalumu zinazoonesha wapigania uhuru wa mwanzo wa Afrika Kusini waliofika Tanzania kuandaa harakati za ukombozi wa nchi yao.
Katika kutekeleza azma hiyo, Serikali ya Tanzania imefanya ukarabati jengo la yaliyokuwa Makao Makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambapo mipango na mikakati yote ya Umoja wa Afrika ya kuzikomboa nchi za Afrika ilifanyika ambalo linatarajiwa kufunguliwa Desemba 2022 ikiwa ni Makumbusho ya Ukombozi wa Afrika.
“Ujenzi wa jengo hili ni utekelezaji wa agizo la Umoja wa Afrika lililotolewa mwaka 2011 kwamba Tanzania itakuwa makao makuu ya Mpango wa Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kwa lengo la kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu zote za harakati za ukombozi na itaungwa mkono na nchi wanachama wa Afrika kwa kila nchi kuwa tawi la kuoneshea historia ya namna walivyopingania harakati za ukombozi wa nchi zao” amesema Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu.
Bw. Yakubu amesema kuwa watanzania wanajivunia ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini na urithi huo ambao umechorwa kwenye kuta za jingo hilo ni ukumbusho unaodhihirisha kuwa nchi hizo ni zaidi ya kaka na dada na hivyo ni muhimu kuhakikisha wananchi wake wanaishi kulingana na maono ya waasisi wake.
“Hakuna kiongozi wa Kiafrika ambaye hajawahi kufika hapa wakati wa mapambano ya ukombozi. Hapa ndipo mahali pekee wapigania uhuru walikuja kutua kupata mbinu, vifaa, mikakati na fedha za kuendesha mapambano ya ukombozi wa nchi zao” amsema Bw. Yakubu.
Naibu Katibu Mkuu Bw. Yakubu ameongeza kuwa kwa upande wa Afrika Kusini, Komredi Oliver Tambo na Water Sesulu hapo ndipo palikuwa nyumbani kwao, kila mara walifanya vikao hapo na ndiyo sababu ya kuchora michoro hiyo kama sehemu ya kuheshimu, kutambua na kuthamini juhudi zao katika eneo walilolipenda na kulipa jina jipya kuwa Maka au Jerusalem.
Tanzania imehusika kwa kiasi kikubwa kwenye kutoa maeneo ya urithi wa ukombozi katika mikoa mingi ikiwa ni pamoja na yale yenye kumbukumbu za Afrika Kusini ya Mazimbu, Dakawa na Kongwa.
Katika maeneo hayo yapo baadhi ya makaburi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini ambayo yamefanyiwa ukarabati katika eneo la Mazimbu na maeneo mengine na kusisitiza kuwa Serikali ya Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kufanya maeneo hayo kuwa eneo la urithi wa kitaifa na yalindwe kisheria ili kuanzisha mchakato wa kutuma maombi kwa UNESCO ili kuzitambua kama urithi wa dunia kwa kuwa yana thamani bora zaidi ya kimataifa.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Michezo, Sanaa na Utamaduni kutoka Afrika Kusini Nocawe Mafu amewashukuru Mzee Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Oliver Reginald Tambo na kusema wachoraji Teboho Elisha Motigoe kutoka Afrika Kusini na Lutengano Mwakipesile kutoka Tanzania wamechora picha ambazo zinawakilisha mambo yaliyofanyika na kupepelekea kuptikana uhuru wa Afrika Kusini.
“Hatuwezi kuzungumzia uhuru wa Afrika Kusini bila kuzungumzia kazi iliyofanywa na Tanzania, nachukua fursa hii kuwashukuru Watanzania kwa mchango wao kwetu. Tunazungumza leo Afrika ya Kusini ipo huru, Nyerere aliruhusu harakati za ukombozi kutoka Afrika Kusini kufanyika Tanzania na kujenga nyumba zao hapa” amesema Naibu Waziri Mafu.
Ameongeza kuwa Nyerere alienda zaidi ya hapo ambapo alitoa ardhi kwa ajili ya watu wa ANC ili kuhakikisha wapigania uhuru hao wanapata maeneo ya kuishi wakati wote wa harakati za ukombozi wa nchi yao katika maeneo ya Mazimbu ambapo walijenga majengo mengi ambayo sasa yanatumika kama kampasi ya Solomon Mahlangu ambayo ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Kilimo Morogoro (SUA), Dakawa pamoja na Kongwa ambapo pia yapo majengo ambayo yanatumika sasa.