***********************
Mkataba wa uzalishaji na ugawanaji mapato (PSA) wa Kitalu cha Ruvuma (chenye leseni mbili, Lindi na Mtwara), ulisainiwa 29 Oktoba, 2005 baina ya Serikali, TPDC na Ndovu Resources (Mkandarasi). Mnamo mwezi Oktoba, 2020, kampuni Ndovu Resource iliuza 50% ya hisa zake kwa kampuni ya ARA Petroleum Ltd na ARA kuwa mwekezaji mkuu katika kitalu hicho. Mkataba huu ulikuwa na vifungu vinavyosimamia mapato iwapo mafuta yatagunduliwa katika kitalu husika, kwakuwa mwekezaji amegundua gesi asilia mkataba wa nyongeza umeandaliwa ili kuongeza vifungu vinavyosimamia mapato ya gesi asilia.
Leo tarehe 25/11/2022 tunafanya hafla ya uwekaji saini katika mkataba wa nyongeza wa mkataba wa awali wa uzalishaji na ugawanaji mapato wa Kitalu cha Ruvuma baada ya kukamilika kwa majadiliano baina ya Timu ya majadiliano ya Serikali na wawekezaji.
Mpaka sasa visima viwili vimechorongwa katika kitalu hiki na kugundua gesi asilia kiasi cha futi za ujazo bilioni 466. Tafiti zinazoendelea zinaonyesha kitalu hiki kina jumla ya kiasi cha gesi cha futi za ujazo bilioni 1,642. Kusainiwa kwa mkataba huu wa nyongeza ni hatua kubwa katika maandalizi ya kuendeleza gesi iliyogunduliwa na hivyo kuongeza uzalishaji wa gesi asilia nchini.
Katika Mradi huu tunakadiria kuwekeza takribani dola za kimarekani milioni 500 katika kuendeleza gesi iliyogunduliwa. Katika uendelezaji na uzalishaji wa Kitalu cha Ruvuma, TPDC inatarajiwa kushiriki kwa 15%. Utekelezaji wa mradi huu unatarajia kuzalisha ajira kwa watanzania pamoja na kukuza uchumi wa nchi yetu kutokana na kodi na tozo mbalimbali zitakazopatikana kutokana mauzo ya gesi. Faida nyingine zitakazopatikana ni pamoja na matumizi ya gesi katika kuzalisha umeme ambayo kwa sasa gesi asili inachangia zaidi ya asilimia sitini (60%) kwenye gridi ya taifa, hivyo utekelezaji wa mradi huu utaongeza kiasi cha umeme unaozalishwa kutokana na gesi asilia, kuendesha viwanda, kutumia majumbani pamoja na kwenye magari.