Wanafunzi wakishuhudia namna ya uaandaaji wa bustani.
Baadhi ya wananchi na viongozi wakishiriki katika uandaajibwa tuta la.bustani ya mboga.
…………………………….
Na ZILLIPA JOSEPH KATAVI
Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi imezindua rasmi kampeni ya kuboresha lishe iliyoambatana na utoaji elimu ya shamba darasa ya jinsi ya kulima bustani za mbogamboga katika shule za msingi kwa lengo la kuinua hali ya lishe ya mkoa wa Katavi ambao kwa mujibu wa taarifa mpaka sasa mkoa huo una asilimia 33.3 ya watoto wanaosumbuliwa na udumavu.
Kampeni hiyo ya kupanda mboga mashuleni itahusisha shule zote 81 za msingi zilizopo wilayani Tanganyika, ambayo inakwenda sambamba na zoezi la utoaji wa chakula cha mchana mashuleni.
Akiizungumza mara baada ya kuzindua kampeni hiyo katika Kijiji cha Bulamata Mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amewataka wazazi kutoona uzito katka suala zima la kuchangia chakula.
‘Kile chakula ambacho mtoto angekula nyumbani mchana kigawe kilete shule ale na wenzie, hii itawajengea watoto upendo na umoja’ alisema Buswelu.
Aidha amewataka viongozi wa ngazi zote kuanzia vitongoji,, vijiji, kata pamoja na viongozi wa dini kushirikiana katika kuhamasisha kaya kuchangia chakula mashuleni.
Afisa Afisa lishe wa Halmashauri ya wilaya ya Tanganyika Nossim Lession amesema wamezindua kampeni hiyo kwa shule za msingi ili kuwezesha wanafunzi kupata chakula chenye mboga mboga sanjari na kupata elimu ya bustani itakayowasaidia kuanzisha bustani zao nyumbani.
Ameongeza kuwa tafiti zinaonyesha kuwa wanafunzi wanaopata chakula shule wanafaulu zaidi kutokana na ukweli kwamba hawapotezi muda kufuata chakula nyumbani na pia utoro unapungua kutokana na wakati kuwa na uhakika wa kula.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Bulamata Nikas Nibengo aliwasihi wananchi kuacha Imani zilizopitwa na wakati za kudharau kula mboga kwa kudhani wataonekana maskini.
‘ Wewe baba ukitoka kwenye kazi zako ukakuta kumepikwa mchicha usigome kula, ukiacha kula na watoto wanakuiga kesho wanakuwa hawapendi mboga mboga matokeo yake udumavu unatutafuna’
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliohudhuria mafunzo hayo wamesema wanajipanga kuanza kuchangia chakula pamoja na kuanzisha kilimo cha mboga katika makazi yao
Mimi Nina kisima kikubwa tu nyumbani nitaanza kupanda mboga nilikuwa sifahamu kama naweza kupanda mchicha popote nimezoea kuona mboga mboga kwenye mabonde’ alisema Asia Bakari mkazi wa Bulamata.