**********************
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kipindi cha kuanzia tarehe 11.11.2022 hadi tarehe 22.11.2022 limefanya Misako ya nguvu na yenye tija katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya na kupata mafanikio ikiwemo kukamata watuhumiwa 03 wakiwa na nyara za serikali, kukamata watuhumiwa 06 wezi wa nishati ya mafuta [Diesel na Petrol] na kukamata watuhumiwa 10 ambao ni wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya na kupatikana na silaha kinyume cha sheria:-
WAKAMATWA KWA KOSA LA KUPATIKANA NA NYARA ZA SEIKALI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia DAVID MARTIN MWAHAYA [40] Fundi Cherehani, Mkazi wa Tabata Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma ya kupatikana na nyara za serikali vipande tisa [09] vya meno ya Tembo vyenye uzito wa Kilogramu 17.4 na thamani ya Tshs 104,908,050/=.
Mtuhumiwa alikamatwa huko Mtaa wa Lubele, Kata ya Ikimba, Tarafa ya Unyakyusa, Wilaya ya Kyela akiwa na vipande hivyo tisa vya meno ya Tembo akiwa amevifunga katika mfuko wa Sulphate akiwa katika harakati za kutafuta mteja.
AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUPATIKANA NA NYARA ZA SERIKALI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia NINDE BUNDALA [78] Mkazi wa Kinyasuguni – Iheha kwa tuhuma za kupatikana na nyara za serikali. Mtuhumiwa alikamatwa huko Kijiji cha Kinyasuguni, Kata ya Iheha, Tarafa ya Madibira, Wilaya ya Mbarali.
Mtuhumiwa alipekuliwa na kukutwa na nyara za serikali ambazo ni:-
- Pembe tatu za Tandala
- Kipande cha Ngozi ya Tandala
- Mafuta yanayodhaniwa kuwa ni ya mnyamapori yaliyohifadhiwa kwenye chupa mbili za plastiki.
Aidha mtuhumiwa alikutwa na silaha mbalimbali za jadi ambazo ni:-
- Mikuki kumi na sita [16].
- Podo lenye mishale sita.
- Upinde mmoja.
Mtuhumiwa ni muwindaji haramu na alikuwa akitafutwa kwa tuhuma ya kujeruhi akiwa na mwenzake aitwaye MATHIDI MBOJE.
WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUPATIKANA NA MALI ZA WIZI.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa sita 1. MRISHO SELEMAN [39] Dereva, Mkazi wa Mbambo 2. VICTOR JULIUS [28] Mlinzi wa Kampuni Kiwike Security 3. CHRISTOPHER HAKIMU [22] Mkazi wa Bwibuka 4. AYUBU VENANCE [27] Mkazi wa Mbambo 5. MESHACK BONIPHACE [22] Mkazi wa Mbambo na ISAYA MWAPASI [20] Mkazi wa Mbambo kwa tuhuma ya wizi wa nishati ya mafuta ya Diesel.
Watuhumiwa walikutwa na nishati hiyo ya mafuta lita 200 ikiwa ndani ya madumu 10 ya lita 20. Aidha watuhumiwa walikamatwa wakiwa na Pikipiki mbili MC.170 DNH Kinglion rangi nyeusi na MC.490 T-Better rangi ya blue Pamoja na madumu tupu 36 ya lita 20.
Watuhumiwa waliiba nishati hiyo ya mafuta ya Diesel katika kambi ya Wachina wanaoendelea na mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Lwanga hadi Tukuyu kwa kiwango cha lami. Watuhumiwa wamefikishwa mahakama ya Wilaya ya Rungwe Novemba 22, 2022.
WAKAMATWA WAKIWA NA DAWA ZA KULEVYA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa kumi [10] ambao ni 1. ISAYA JULIUS [28] 2. ASHERY JOFREY [24] 3. GISBERT MCHILO [30] 4. JAMSON FURAHA [25] 5. EMANUEL JOSEPH [22] 6. BRYTON MKONDYA [24] 7. SALUM MASANJA [29] wote wakazi wa Itumbi, 8. ZAWADI MWAMPASHI [26] na 9. EMANUEL FRANK [21] wote wakazi wa Matondo kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya Bhangi Debe 02, Kete 293 na Gramu 30.
Watuhumiwa ni wauzaji na watumiaji na dawa hizo za kulevya, watafikishwa mahakamani upelelezi utakapokamilika.
AKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUPATIKANA NA SILAHA.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia YOHANA MASUDI [25] Mkazi wa Kitongoji cha Mkwajuni akiwa na silaha bunduki moja aina ya Shot Gun yenye namba za usajili 44362 na risasi moja kinyume cha sheria.
Aidha katika upekuzi uliofanywa nyumbani kwa mtuhumiwa alikutwa na mali mbalimbali za wizi ambazo ni:-
- TV moja aina ya Zunne inchi 28 na remote yake.
- Remote moja ya King’amuzi cha Azam
- Redio Subwoofer aina ya Sundar
- Solar Panel moja ya Watt 120
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishna Msaidizi wa Polisi Benjamin Kuzaga anatoa wito kwa wananchi kuacha kuhujumu miradi ya serikali ambayo inajengwa katika maendeleo mbalimbali kwa kuiba au kuharibu. Aidha anatoa wito kwa jamii kuachana na biashara haramu kwani Jeshi la Polisi halitamvumilia mtu yeyote Yule kwa kitendo chochote cha uhalifu au uvunjifu wa amani.