*************
Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dar es Salaam
Sekta ya Ubunifu na Filamu katika nchi za Tanzania na Afrika Kusini inakuwa kwa kasi na inawaajiri vijana wengi na inatoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuongeza pato la taifa.
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa upande wa Tanzania na Wizara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni kutoka Afrika Kusini wameandaa Semina hiyo ikiwa ni sehemu ya Tamasha la Msimu wa Utamaduni wa Afrika Kusini na Tanzania ni maalumu kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuwajengea uwezo wasanii, waandaaji na wasambazaji wa filamu imefanyika Novemba 23, 2022 jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa Mkumbusho ya Taifa hatua ambayo inayosaidia kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
Semina hiyo imeandaliwa mahususi kuwaongezea chachu na kuwahamasisha vijana kuendelea kufanya kazi za Sanaa ikiwemo filamu ili kukuza uchumi wao na kuongeza pato la taifa.
Miongoni mwa mada zilizojadiliwa katika semina hiyo ni Mpango wa Serikali katika kuunga mkono Sekta ya Ubunifu ambayo ilitolewa na Naibu Mkurugenzi Mkuu, Idara ya Michezo, Sanaa na Utamaduni kutoka Afrika Kusini Dkt. Cynthia Khumalo na Sekta ya Ubunifu wa Utamaduni Tanzania ambayo ilitolea na Angela Kilusungu, Meneja Programu wa Uchumi na Ubunifu kutoka taasisi ya Utamaduni na Maendeleo ya Afrika Mashariki (CDEA).
Mada nyingine ni Sekta ya Ubunifu wa Kitamaduni na Utafiti wa Utamaduni wa Afrika Kusini katika kukuza uchumi na ubunifu ambayo imetolewa na Bi Amy-Louise Shelver na Bi Masilakhe Njomane ambao ni Waangalizi wa Utamaduni wa Afrika Kusini, Matumizi ya mifumo ya biashara katika sekta ya Utamaduni na ukuzaji wa uchumi kwa njia ya ubunifu ambayo imetolewa na Bw. Hatibu Madudu, Mtayarishaji wa Maudhui na Mkurugenzi ukuzaji wa Vipaji kutoka kampuni ya Multichoice pamoja na mada ya Uchumi wa Urithi Eneo la SOMAFCO kuhusu Africa ijayo ambayo imetolewa na Bw. Andile Skosana kutoka kampuni ya CityConsolidator Africa (Pty) Ltd.
Tamasha hilo linafanyika nchini kunzia Novemba 16 hadi Desemba 4, 2022 ambapo limefanyika katika maeneo Dar es salaam, Dodoma, Morogoro na linatarajiwa kuhitimishwa Zanzibar.