Uongozi wa TIRA ukiendelea kutoa elimu ya bima kwa wananchi kweye Maadhimisho ya wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea kufanyika Kitaifa katika viwanja vya Rock City Mall Jijini Mwanza
Kaimu Meneja wa TIRA Kanda ya ziwa Richard Toyota akiwahimiza Wananchi kufika kwenye banda lao ili wapate elimu ya bima kwenye Maadhimisho ya wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea kufanyika Kitaifa Jijini Mwanza
Meneja wa maendeleo ya soko la Bima kutoka TIRA Stella Rutaguza akielezea namna wanavyoendelea kutoa elimu ya bima kwa wananchi
***************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imewaomba Wananchi kufika kwenye banda lao ili waweze kupata elimu ya bima katika wiki ya Huduma za Fedha inayoendelea kuadhimishwa Kitaifa Jijini Mwanza.
Ombi hilo limetolewa leo Jumanne Novemba 22, 2022 na Kaimu Meneja wa Mamlaka ya usimamizi wa bima Kanda ya ziwa (TIRA) Richard Toyota, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Toyota amesema Maadhimisho ya wiki ya fedha ni fursa kwa wananchi kwani watapata elimu mbalimbali ikiwemo ya bima.
Amesema Wananchi wanapokuwa wanafanya shughuli zao mbalimbali za kiuchumi wakiwa na bima wanakuwa na usalama zaidi kutokana na bima kuwa kinga ya vitu vyao.
Kwa upande wake Meneja wa maendeleo ya soko la Bima kutoka (TIRA) Stella Rutaguza, amesema wananchi watakapofika katika Banda leo watapata fursa ya kueleweshwa umuhimu wa bima aina mbalimbali na bidhaa za bima zilizopo kwenye makampuni yao sanjari na kuwaelimisha kuhusu haki na wajibu wao juu ya taratibu za kufuata pale wanapokuwa na madai ya bima.
” pamoja na programu ya Serikali ya kutoa elimu ya fedha sisi kama TIRA tumekuwa nautaratibu wa kutoa elimu mbalimbali za bima hatua iliyosaidia ongezeko kubwa la Wananchi kuwa na uelewa wa umuhimu wa bima na wamefanikiwa kujiunga na bima za hiari ikiwemo bima ya nyumba” amesema Rutaguza
Ametoa rai kwa wananchi ambao hawajajiunga na bima wajiunge na bima za hiari ambazo zitakuwa ni faida yao katika uchumi endelevu.