Meneja wa Ruwasa wilaya ya Songea Mathias Charles akitoa taarifa ya mradi wa maji unaokwenda kutekelezwa katika kijiji cha Mtyangimbole Halmashauri ya Maadaba wenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni 5.5.
Meneja wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma Rebman Ganshonga akieleza mikakati ya Ruwasa katika utekelezaji wa miradi wa maji katika mkoa huo kwenye hafla fupi ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji Mtyangimbole Madaba.
Meneja wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma Mhandisi Rebman Ganshonga akimuonesha Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema wa pili kulia na Katibu Tawala wa mkoa wa Ruvuma Stephen Ndaki wa kwanza kushoto na Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Clement Kivegilo katikati michoro ya mradi wa maji Mtyangimbole ambapo utakapokamilika utahudumia zaidi ya wakazi 14,000 wa kata ya Mtyangimbole na Gumbiro.
Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegilo kulia na Mwakilishi wa Kampuni ya Namis Corporate Ltd Honest Uiso wakionyesha mikataba baada ya kusaini mkataba wa ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Mtyangimbole utakaohudumia zaidi ya wakazi 14,000 wa kata ya Mtyangimbole na Gumbiro Jimbo la Madaba.
Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegilo akizungumza mara baada ya utiaji saini wa mkataba ujenzi wa mradi wa maji Mtyangimbole.
Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema,akizungumza na wakazi wa kijiji cha Mtyangimbole wilayani humo baada ya utiaji saini wa mktaba wa ujenzi wa mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya zaidi ya Sh.bilioni 5.5.
……………………………
Na Muhidin Amri,Songea
WAKALA wa usambazaji maji na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),umesaini mkataba mmoja wa ujenzi wa mradi wa maji wenye thamani ya Sh.bilioni 5.5 utakaohudumia zaidi ya wakazi 14,000 wa vijiji vya Mtyangimbole,Likarangilo na Luhimba Halamshauri ya wilaya Madaba mkoani Ruvuma.
Akizungumza mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo katika kijiji cha Mtyangimbole Mkuu wa wilaya ya Songea Pololet Mgema alisema,mkataba huo unaonyesha kuwa tatizo la maji katika kata ya Mtyangimbole na Gumbiro lililokuwepo tangu Uhuru linakwenda kumalizika.
Amemtaka Mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo kampuni ya Namis Corporate Ltd, kwenda kufanya kazi usiku na mchana ili kazi hiyo iweze kukamilika haraka kama ilivyo kwenye makubaliano ya mkataba.
Mgema aliyemwakilisha Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanal Laban Thomas alisema,wakazi wa vijiji hivyo vinavyounda kata za Mtyangimbole na Gumbiro wana kiu kubwa ya kupata huduma ya maji safi na salama na siyo maneno maneno kama ilivyozoeleka.
Alisema,kwenye utekelezaji na usimamizi wa miradi ya maji vinahitajika vitendo zaidi ili Serikali ijivunie kufanya kazi na wakandarasi wazawa ambao watatekeleza miradi ya maji kwa kushirikiana na wataalam wake.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo,amemtaka Mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana na amemhakikishia malipo na stahiki zote zimekamilika na kinachosubiriwa kwa sasa ni kuanza kazi hiyo.
Kivegilo,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kutoa fedha kwa Ruwasa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kuhaidi kwamba, fedha zote zinazotolewa na Serikali ya awamu ya sita zitafanya kazi iliyokusudiwa.
Aidha amemwambia Mkuu wa wilaya kuwa,Ruwasa itafanya kazi karibu na wakandarasi wote bila kuchoka hadi pale watakapo tekeleza ahadi ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kumtua mama ndoo kichwani.
Katika hatua nyingine Mhandisi Kivegilo,amempongeza Meneja wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma Rebman Ganshonga na wasaidizi wake kwa matumizi sahihi ya fedha na kutekeleza miradi ya maji kwa wakati,hivyo kupunguza kero ya maji kwa wananchi.
Amemtaka mkandarasi kuhakikisha anawatumia wananchi hasa vijana katika kufanya kazi mbalimbali zisizohitaji utaalam mkubwa ikiwamo kuchimba mitaro ili jamii ya eneo hilo iweze kunufaika kuwepo kwa mradi huo.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Songea Mhandisi Mathias Charles alisema,awali mradi huo uliibuliwa na wananchi wa kata hizo kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.
Alisema,chanzo kikuu kipo katika wilaya ya Namtumbo katika safu ya milima ya Motogoro ambacho kina uwezo wa kuzalisha lita 1,883,562.16 kwa siku na mahitaji ya wananchi ni lita 633,621.15 hivyo kuwa na ziada ya lita 1,249,941.01.
Hata hivyo alisema,wananchi waligundua kuwa wanahitaji msaada wa kitaalam kutoka Ruwasa ili wajengewe miundombinu ya kisasa inayoendana na matakwa ya Serikali na tayari walisha changa Sh.milioni 19 ambazo zilitumika kuanza na ujenzi wa banio kama hatua ya kwanza ya utekelezaji wake.
Diwani wa kata ya Mtyangimbole Erick Mkolwe alisema,wananchi wa Mtyangimbole watatoa ushirikiano mkubwa kwa wataalam wa Ruwasa na Mkandarasi wa mradi huo kwa kuwa wamechoka kusubiri huduma ya maji safi na salama kwa muda mrefu.