KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Gilbert Kalima,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu uchaguzi wa nafasi mbalimbali za jumuiya hiyo ngazi ya taifa utakaofanyika Novemba 24-25, mwaka huu jijini Dodoma.
………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Gilbert Kalima,amesema kuwa wajumbe 893 kutoka Mikoa yote nchini watashiriki kufanya uchaguzi wa viongozi wa jumuiya hiyo jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi wa nafasi mbalimbali za jumuiya hiyo ngazi ya taifa utakaofanyika Novemba 24-25, mwaka huu jijini Dodoma.
Bw.Kalima amesema kuwa wajumbe 893 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watashiriki kwenye mkutano huo na kuwa maandalizi yote yako tayari.
“Viongozi wanaotarajiwa kuchaguliwa ngazi ya taifa ni nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ngazi ya taifa, ambaye pia atakuwa Mjumbe wa Kamati kuu ya CCM, nafasi nyingine ni Makamu Mwenyekiti wa jumuiya ambaye atakuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa nafasi yake, zingine ni nafasi tano za wajumbe wa NEC, ambapo tatu kutoka Tanzania bara na mbili Zanzibar, pia kutakuwa na Wajumbe wa Baraza Kuu la Wazazi taifa nafasi sita zitagombewa, uwakilishi wa jumuiya zingine ngazi ya taifa,”amesema Bw.Kalima
Amesema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ya uchaguzi huo ni wazazi chimbuko bora la malezi kwa kuwa mpango kazi wa miaka mitano ijayo wamejipanga kusimamia ipasavyo maadili nchini na kutoa kipaumbele kwenye masuala ya mazingira.