**********************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
CHAMA cha wachimbaji madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani, limemuaga Afisa madini mkazi Mirerani (RMO) Fabian Mshai kwa kumkabidhi tuzo iliyotukuka kutokana na utendaji kazi wake.
RMO Fabian ambaye ni Afia madini wa mkoa wa kimadinin wa Simanjiro, anaenda kusomea shahada ya pili chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) amewaaga wadau wa madini kwenye tafrija iliyofanyika ukumbi wa Mazubu Grand Hotel mji mdogo wa Mirerani.
Katibu wa MAREMA Tawi la Mirerani, Rachel Njau akizungumza kwenye tafrija hiyo ameeleza kuwa wameamua kumkabidhi tuzo iliyotukuka RMO Fabian ili kutambua mchango wake kwa muda wa miaka miwili aliyowatumikia wachimbaji.
Rachel amesema RMO Fabian amekuwa na mafanikio makubwa kwenye utumishi wake wa miaka miwili wa nafasi hiyo hivyo wameona wampe tuzo hiyo ya heshima iliyotukuka.
“Kwa muda wa miaka miwili aliyokaa kwenye nafasi hiyo ameongoza ofisi ya madini kwa haki bila kumuonea mtu na kuwatetea wachimbaji wadogo hivyo anastahili kupata tuzo ya heshima,” amesema Rachel.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani, Adam Kobelo amesema RMO Fabian mara zote alikuwa anawatetea wachimbaji wadogo ili kuhakikisha uchumi wao unakuwa mzuri.
Mmoja kati ya wamiliki wa mgodi wa madini ya Tanzanite Fatuma Kikuyu amemkabidhi RMO Fabian, kitabu kitakatifu cha Biblia na taji ili kuonyesha kuthamini mchango kwa wachimbaji.
Akizungumza kwenye tafrija hiyo RMO Fabian amewashukuru MAREMA Tawi la Mirerani kwa kumpatia tuzo hiyo kwani imempa imani kubwa na kumbukumbu isiyofutika kwenye maisha yake.
“Kama unafanya kazi kwenye jamii na wao wakaona unafanya jambo kubwa na kukupatia tuzo unapaswa kushukuru tangu mwaka 2017 nilipokuja Mirerani, miaka mitatu nikiwa afisa wa kawaida na miaka miwili nikiongoza ofisi,” amesema RMO Fabian.
Amesema hivi sasa anaenda chuo kikuu cha UDOM Jijini Dodoma kuongeza elimu hivyo wadau wa madini wampe ushirikiano wa kutosha RMO mwingine atakayefika badala yake.
Hata hivyo, MAREMA Tawi wamewakabidhi vyeti vya kutambua mchango wao kwenye sekta ya madini, baadhi ya kampuni ikiwemo Bilionea Saniniu Laizer, Bilionea Anselm Kavishe, Franone Ltd, Chusa Mining na God Charity.