Na Mwandishi wetu, Babati
KATIBU mstaafu wa UWT wa Wilaya za Babati, Kondoa na Arusha mjini na Mikoa ya Arusha na Rukwa Fatuma Tsea amechaguliwa kwa kura za kishindo kuwa Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Manyara.
Fatuma Tsea mwenye uzoefu mkubwa wa uongozi uliobobea kwenye jumuiya ya UWT, amewabwaga wanawake wenzake wengine watatu waliokuwa wanawania nafasi hiyo.
Akizungumza baada ya kuchaguliwa kwa kura za kishindo Tsea ameahidi kuwatumikia wanawake wa Manyara ila ameomba wampe ushirikiano wa kutosha.
Mwenyekiti huyo wa UWT Mkoa wa Manyara, ambaye nyumbani kwao ni Wilaya ya Hanang’ amesema wanawake wa Manyara wakiendeleza mshikamano watapiga hatua kubwa.
Hata hivyo, amewapongeza wabunge wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara, kwa kutowaelekeza wajumbe ili kuwachagua wagombea wanaowataka wao.
Amesema wabunge wa viti maalum wa mkoa wa Manyara, Regina Ndege na Yustina Rahhi hawakuwaelekeza wajumbe wawachague wagombea wao hivyo wanapaswa kupongezwa.
“Pia mbunge wa vijana Taifa kupitia mkoa wa Manyara, Asia Halamga ambaye ni mpiga kura wetu naye hakuwa na wagombea kwenye uchaguzi huu wote wamewaacha wanawake wachague mtu wanayempenda,” amesema Tsea.
Mkuu wa wilaya ya Mbulu, Sezaria Makota ambaye ni msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, amemtangaza Tsea kushika nafasi hiyo kwa kupata kura 284.
Makota amesema Claudia Haule amepata kura 38 Diana Kulo amepata kura 31 na Mariam Njavike amepata kura nne.