Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akihutubia katika mkutano wa tano (5) wa mashirikiano kati ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) ya Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi (SMZ) uliofanyika kisiwani Unguja.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, akisisitiza jambo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi kutoka SMT, Ludovick Nduhiye (kushoto), na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Mhe. Masoud Ali Mohammed, kisiwani Unguja.
Katibu Mkuu wa Ardhi, Maendeleo na Makaazi (SMZ), Dkt. Mngereza Miraji (kulia), akibadilisha hati za makubaliano na Naibu Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi kutoka SMT, Ludovick Nduhiye (kushoto), katika mkutano wa tano wa mashirikano baina ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (SMT) na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ardhi, Maendeleo na Makazi (SMZ), uliofanyika kisiwani Unguja.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Ludovick Nduhiye (kulia), akiteta jambo na Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango kutoka Sekta hiyo, Richard Mkumbo (kushoto), wakati wa mkutano wa tano wa mashirikiano baina ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (SMT) na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ardhi, Maendeleo na Makazi (SMZ), uliofanyika kisiwani Unguja.
Watendaji wa Taasisi kutoka Bodi ya Usajili ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) ya SMT na Bodi ya Usajili ya Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo (AEQSRB) ya SMZ wakisaini hati za makubaliano ya mashirikiano kati ya taasisi hizo katika mkutano wao wa tano baina ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (SMT) na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ardhi, Maendeleo na Makazi (SMZ), uliofanyika kisiwani Unguja.
Watendaji wa Taasisi kutoka Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB) ya SMT na Bodi ya Usajili ya Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji Majengo (AEQSRB) ya SMZ wakisaini hati za makubaliano kati ya taasisi hizo katika mkutano wao wa tano baina ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (SMT) na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ardhi, Maendeleo na Makazi (SMZ), uliofanyika kisiwani Unguja.
Watendaji wa Taasisi kutoka Bodi ya Usajili ya Wakandarasi (CRB) ya SMT na Bodi ya Usajili ya Wakandarasi Zanzibar (ZCRB) ya SMZ wakisaini hati za makubaliano kati ya taasisi hizo katika mkutano wao wa tano baina ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (SMT) na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ardhi, Maendeleo na Makazi (SMZ), uliofanyika kisiwani Unguja.
Watendaji wa Taasisi kutoka Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) ya SMT na Wakala wa Barabara Zanzibar (ZANROADS) ya SMZ wakibadilishana hati za makubaliano ya mashrikiano kati ya taasisi hizo katika mkutano wao wa tano baina ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (SMT) na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ardhi, Maendeleo na Makazi (SMZ), uliofanyika kisiwani Unguja.
……………………………..
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa, ameishauri Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na Wizara ya Ardhi, Maendeleo na Makazi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), kuwekeza na kutoa fursa za kazi kwa vijana katika miradi ya ujenzi bara na visiwani ili kuwajengea uwezo wataalam wao wa ndani.
Amezungumza hayo kisiwani Unguja – Zanzibar, wakati akifunga mkutano wa tano wa mashauriano baina ya Wizara yake na Wizara hizo zinazoshabihiana katika majukumu ya taasisi zao na kusisitiza kudumisha ushrikiano baina yao ili kubadilishana uzoefu na kuongeza chachu katika mabadiliko chanya ya kiutendaji.
“Nchi yetu ina fursa nyingi, miradi mingi na hizi fursa tulizopata tuzitumie kwa kuwapa vijana kutoka bara na visiwani ili nchi yetu iweze kujenga watu katika usimamizi na ujenzi wa miundombinu bora na ya kisasa”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Aidha, Prof. Mbarawa amesema kupitia Wizara yake inaendelea na mkakati wa kuwajengea uwezo wataalam wake kwa kuwashirikisha kwenye miradi mikubwa mbalimbali ikiwemo ya ujenzi wa viwanja vya ndege, barabara na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).
“Wizara imepeleka wataalam mbalimbali katika miradi mikubwa ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Msalato, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), uboreshaji wa bandari, ujenzi wa meli na ujenzi wa barabara ya mzunguko (ring road) iliyopo Dodoma yote hii ikiwa ni kuwatengeneza vijana kuwa wabobezi katika kila eneo”, amefafanua Prof. Mbarawa.
Pia, amezishauri Wizara hizo ziweke mikakati ya kuongeza na kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika kazi za ujenzi ambapo ushiriki wa kundi hilo bado hauridhishi.
“Nitoe wito kwa wenzetu wa SMZ kuweka juhudi katika kulisaidia kundi hili muhimu ili liweze kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa shughuli za ujenzi kwani lengo ni kukuza uchumi kuanzia ngazi ya familia kwasababu ukimkomboa mwanamke kiuchumi, unakuwa umeikomboa familia nzima”, amefafanua Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa ametoa msisitizo kwa Wataalam wa Sekta ya Ujenzi kuhakikisha kazi zinafanyika kwa wakati na kwa ubora ili thamani ya fedha ipatikane na hatimaye watanzania waweze kujengewa miundombinu bora na ya kisasa.
Awali akifungua mkutano huo wa mashirikiano baina ya Wizara hizo, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukzui, Mhe. Masoud Ali Mohammed, ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, amewataka wataalam hao kujifunza kutoka pande zote mbili za Muungano namna ambavyo wanatekeleza majukumu mbalimbali na hivyo kuyachukua yale mazuri kwa lengo la kuboresha katika utendaji kazi.
Katika mkutano huo Mawaziri hao wameshuhudia utiaji wa saini wa hati mbili za makubaliano, moja ikiwa baina ya Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi (SMZ) na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi – SMT) kuhusu Bodi za usajili wa wataalam wa sekta ya ujenzi na ya pili ni baina ya Taasisi ya Teknolojia ya Ujenzi (ICoT) na Wakala wa Barabara Zanzibar (ZANROADS).
Mkutano wa tano wa mashirikano baina ya taasisi za Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (SMT) na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na Wizara ya Ardhi, Maendeleo na Makazi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imefanya vikao kuanzia ngazi ya wataalam, ngazi ya Makatibu Wakuu na ngazi ya Mawaziri ambapo pamoja na mambo mengine watalaam walipata fursa ya kutemebelea na kubadilishana uzoefu katika baadhi ya miradi inayosimamiwa na Wakala wa Barabara Zanzibar (ZANROADS) na Wakala Majengo Zanziba (ZBA).