Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mwenyekiti wa umoja wa vijana Mkoani Pwani ( UVCCM) aliyekuwa akitetea nafasi yake ,Samaha Said amewaasa vijana kukomaa kisiasa na kuachana na siasa za chuki na kuchafuana.
Aliyayasema hayo baada ya kumalizika uchaguzi wa vijana Mkoani humo uliofanyika Picha ya Ndege Mjini Kibaha.
Samaha alieleza, ni bora kutengeneza kwenye siasa na kufanya siasa lakini waache chuki na kuchafuana ili kujiimarisha Jumuiya.
“Siasa ya vijana ni ndefu hivyo wasipende kuchafuana maana hawajui yule wanae mchafua atakuwa nani hivyo chuki na fitina zisiwepo bora tusema twende salama,”alisema Samaha.
Hata hivyo alieleza, kwa upande wa vijana hakuna maslahi binafsi bali ni kwa ajili ya chama na kazi za chama zinajulikana na kuwa uchaguzi umeisha kilichobaki ni kuitengeneza jumuiya na chama.
“Tushirikiane kukijenga chama tusameheane kwani hii itatufikisha pale tunapotaka kufika mmenikopesha imani nitawalipa imani hiyo kwani mmenipa kura nyingi,”alisema Samaha.
Vilevile alieleza, ataendelea kuleta mabadiliko na kuunganisha Jumuiya ili kuleta maendeleo na kuwataka kuachana na makundi .
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo msimamizi wa uchaguzi Fatuma Ndee alimtangaza Samaha Said kuwa mshindi kwa kupata kura 223, akifuatiwa Adam Salehe Athuman aliyepata kura 204, Tengeneza Abuu kura tatu na Mkongo Mauli kura mbili.
Naye mjumbe wa baraza kuu la mkoa kuwakilisha Taifa Juma Kwangaya alisema kuwa ajenda za vijana kutoka mkoa Pwani ataziwasilisha sehemu husika ili kuleta maendeleo.
Naye Katibu wa (UVCCM) Kisamba Kidando alifafanua, uchaguzi huo umefuata taratibu zote hadi kufanikiwa kupata viongozi na hakukuwa na malalamiko yoyote.
Kidando alisema, kikubwa ni kuwapa ushirikiano viongozi waliochaguliwa ili malengo waliyoyaweka yaweze kutimia na kuufanya umoja huo kuwa imara kwani ni nguzo imara ndani ya chama.