Klabu ya Rotary ya Dar es Salaam, imeendele kuchangia katika maendeleo ya elimu nchini kwa kutoa madawati kwa shule zenye uhaba wa madawati nchini ambampo imekabidhi madawati mapya 100 kwa shule ya msingi Mwananyamala ya jijini Dar es Salaam na kutimiza idadi ya jumla ya madawati 1,700 yenye thamani ya Zaidi ya shilingi Milioni 250 ambayo klabu hiyo imeshatoa kwa shule mbalimbali hapa nchini.
Madawati hayo yalikabidhiwa na wanachama wa klabu hiyo wakiongozwa na Gavana wa Klabu za Rotary kwa nchi za Uganda na Tanzania Peace Teremwa na kupokelewa na mbunge wa Kinondoni Tarimba Abbas Novemba 16 mwaka huu katika shule hiyo iliyopo Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo, Rais wa klabu hiyo Nikki Aggarwal, amesema klabu hiyo imekuwa ikishirikiana na jamii katika kuboresha huduma za jamiikwa kuendesha miradi mbalimbali ya kijamii ambapo kwa sasa mradi wao mkuu ni wa kutoa madawati kwa shule zenye uhitaji.
Amebainisha kuwa mradi huo unaenda sambamba na zoezi la upandaji miti ili kuhifadhi mazingira. “Hadi sasa mradi huu umeshatoa madawati 1,700 yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 250 kwa shule mbalimbali. Tunafurahi sana kuona kuwa mradi huu umekuwa wa manufaa makubwa kwani umewatoa wanafuzi 500 kwenye adha ya kukaa kwenye sakafu wakati wakiwa darasani.”
Amesema kuwa kwakuwa moja ya malighafi katika kutengeneza madawati ni mbao, mradi huo unaenda sambamba na upandaji wa miti ili kutunza mazingira.
Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea madawati hayo, Mbunge waKinondoni Tarimba Abbas, amesema Jimbo Kinondoni ni miongoni mwa majimbo zinazohitaji madawati kwani kumekuwa na ongezeko la wanafunzi wanaoandikishwa shuleni kutokana na sera ya serikali ya kutoa elimu bure.
Amesema msaada huo wa madawati huo ni muhimu sana kwani na umekuja kwa wakati muafaka kwani utaisaidia serikali kutumia fedha ambazi zingenunulia madawati kuimarisha miundombinu mingine katika shule zetu.
Ameipongeza Klabu ya Rotary kwa kazi kubwa inayofanya kusaidia jamii katika sekta mbalimbali za kijamii na ameihakikishia ushirikiano wa hali na mali ili kufanikisha malengo ya kuleta maendeleo kwa jamii yetu.