Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba akizungumza na waandishi wa habari
Mkuu
wa Mkoa wa Tanga Omari Mgumba akizungumza na waandishi wa habari katika
viwanja vya CCM Mkwakwani Jijini Tanga ambacho pia kitatumika katika
mashindano ya Shimuta
Mwenyekiti wa SHIMUTA Taifa Roselyne Massam akizungumza kuhusu maandalizi ya mashindano hayo yanayoanza leo Jijini Tanga
Mratibu Mkuu wa Shirikisho hilo Maswet Masinde alieleza namna
walivyojipanga kuhakikisha hakuna mamluki atakayechezeshwa kwenye timu
zitakazoshiriki mashindano hayo kwani wamejipanga kusimamia sheria
kanuni na taratibu zinazowaongoza katika michezo yote.
Na Oscar Assenga,TANGA.
MAKAMU wa Rais Dkt Philip Mpango
anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mashindano ya Mashirika
ya Umma,Makampuni na Taasisi Binafasi nchini (Shimuta) Novemba 21 mwaka
huu kwenye viwanja vya Mkwakwani Jijini Tanga.
Hayo
yalibainishwa leo na Mwenyekiti wa SHIMUTA Taifa Roselyne Massam wakati
akizungumza na waandishi wa habari mjini Tanga kuhusu mashndano hayo
ambapo alisema kwa mara ya kwanza tokea yalipoanza mwaka huu 2022
yameweka rekodi mpya.
Alisema rekodi hiyo inatokana na kuongezeka
kwa idadi ya timu na sasa kufikia 52 zitakazochukua kuwasaka mabingwa
kupitia michezo watakayoshindaniwa ambayo itatimua vumbi leo Novemba 15
katika viwanja mbalimbali Jijini hapa
Mwenyekiti huyo
alisema amesema tangu wameshika hatamu ya kuliongoza shirikisho hilo
haijawahi kutokea kushirikisha timu nyingi zaidi kama mwaka huu jambo
ambalo linaonyesha mwitikio umekuwa ni mkubwa na michezo hiyo kuonekana
kuleta tija kwa washiriki mashirika, makampuni na taasisi zenyewe
wanazotoka.
Naye kwa upande wake Mratibu Mkuu wa Shirikisho
hilo Maswet Masinde alieleza namna walivyojipanga kuhakikisha hakuna
mamluki atakayechezeshwa kwenye timu zitakazoshiriki mashindano hayo
kwani wamejipanga kusimamia sheria kanuni na taratibu zinazowaongoza
katika michezo yote.
Mashinde alisema kwamba msimu huu wamekuwa
wakali zaidi kuhakikisha wanadhibiti mamluko hivyo wamekwisha kufanya
uhakiki kuondoa mamluki kwa kutumia taasisi za umma ikiwemo NHIF, WCF,
PSSF kuhakiki washiriki lengo likiwa ni michezo hii iwe ni kwaajili ya
watumishi wale ambao wanatambulika kisheria na ili uwe mshiriki unapewa
leseni maalumu na lazima uwe umehakikiwa kwenye mifuko hiyo.
Mratibu
huyo alisema kwamba mpaka sasa wanamichezo 2183 ambao tayari
wameshafika hapa jiji la Tanga na ni namba kubwa ya wanamichezo
wanaoshiriki lakini tuna kanuni ambazo zinaongoza katika mashindan pia
watatumia kanuni za michezo husika pale inapobidi huku akisisitiza
umuhimu wa waamuzi wasimamie sheria taratibu na miongozo inayoongoza
michezo husika ili kusiwepo na manung’uniko ya hapa na pale
Akieleza
namna mkoa huo ulivyojipanga kuelekea Mashindano hayo Mkuu wa Mkoa wa
Tanga Omari Mgumba amesema kwamba mkoa upo salama na kuwahakikishia
ulinzi na usalama muda wowote watakapokuwepo kwenye mashindano hayo.
Mkuu
huyo wa Mkoa alitumia nafasi hiyo pia kuwataka wakazi wa Tanga wakiwemo
wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo wadogo kuchangamkia fursa za
uwepo wa mashindano hayo kujiongezea kipato.
“Mashindano haya
ni zaidi ya michezo yana faida ya kipato lakini yanainua uchumi wa mtu
mmoja mmoja na kuongeza pato la taifa, nitoe wito kwa wafanyabiashara
wote wachangamikie fursa na kujitokeza kwa wingi katika michezo hii “
alisema Mgumba.
“Suala la hali ya ulinzi na usalama liko
vizuri tumeendelea kuimarisha doria kwa sababu tumepata ujio wa watu
wengi hivyo hali ya usalama iko vizuri tumeendelea kujiimarisha zaidi
doria za mchana na usiku kuwahakikishia wanamichezo na wageni wetu wote
wanakuwa salama wakati na hata baada ya kumaliza michezo” aliongeza
Michezo
itakayochezwa wakati wa mashindano hayo ni michezo ya mpira wa miguu
kwa wanaume, mpira wa Pete , Wavu, Kikapu, Dats, Pool table, Vishale ,
Draft kukimbia kwa magunia, Riadha kuvuta kamba Bao na mingineyo
kedekede, lengo kuu hasa ikiwa ni kuimarisha mahusiano baina ya taasisi,
mashirika na makampuni kuimarisha afya kupitia michezo ikiwa pia ni
kuondokana na magonjwa yasiyoambukiza.
Michezo hiyo ambayo
hufanyika kila mwaka ni kwa mara ya pili mfululizo kufanyika ndani ya
mkoa wa Tanga mwaka huu yakija na kauli mbiu ya ‘SHIMUTA familia moja’.