**************************
Na Mwandishi wetu, Babati
Vita ya kutaka kuwinda wanyamapori baina ya makampuni yameingiza katika mgogoro Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Burunge, Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara, baada ya Spika wa Jumuiya hiyo kutangaza Kitalu cha uwindaji kipo wazi bila ridhaa ya Bodi ya wadhamini .
Wakati spika akiwa amesaini barua ya kutangaza Kitalu hicho kutaka kampuni kuomba kuwinda ,tayari Bodi ya jumuiya hiyo Julai 14,2022 ilisaini Mkataba kuendelea na mwekezaji kampuni ya uwindaji wa kitalii ya EBN ambayo kwa kiasi kikubwa inafanya Utalii wa picha ambao ni rafiki kwa uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.
Mkataba huo, umesainiwa na Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini, Patricia Mosea, Katibu wa Burunge WMA, Benson Mwaise na Mkurugenzi wa EBN, Nicolas Negre baada ya kutolewa baraka na Wizara ya Maliasili na Utalii baada ya tathimini na viongozi serikali na halmashauri ya Babati.
Hata hivyo, katika mgogoro huo, Spika wa Jumuiya hiyo, Hamis Juma amekuwa akitaka Kitalu hicho, kinachopakana na hifadhi ya Tarangire kupewa Kampuni ya nyingine ya uwindaji jina linahifadhiwa ambayo imekuwa ikitaka eneo hilo ikisaidiwa na baadhi ya vigogo wa Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari Juma amekiri kuwepo na mgogoro katika jumuiya hiyo hata hivyo alikataa kufafanua ni kwanini anapingana na Bodi ya wadhamini na secretariet ya jumuiya hiyo na viongozi wa Serikali walioshiriki mchakato wa kusaini mkataba mpya.
Juma ambaye anatajwa kuwa na ukwasi mkubwa katika siku za karibuni amesema jambo hilo lipo ngazi za juu huku akisisitiza mkataba uliosainiwa awali na viongozi wa jumuiya ulikuwa na mapungufu.
Hata hivyo, mjumbe mmoja wa bodi ambaye ameomba kuhifadhiwa jina ametaka kuchunguzwa Spika huyo kwani amevunja sheria za WMA kwa kutoa taarifa potofu kuwa Kitalu kipo wazi wakati akijua wamesaini mkataba na alihudhuria siku ya kusainiwa mkataba huo.
“Kwenye ule mkataba tuliosaini upo wazi kuwa kama tulitaka kuchukuwa Kitalu tunapaswa kutoa taarifa miezi mitatu kabla kwa kuwa kuna uwekezaji pale na tayari kuna watalii wamelipa Sasa anatumiwa na watu kutuvuruga na kuvuruga utalii,” amesema.
Amesema tayari mgogoro huo ulifikishwa Taasisi ya Kuzuia na kupambana na rushwa na tayari wao kama wajumbe wa bodi wamehojiwa na spika huyo.
Amesema Spika huyo pia amekuwa akitamba kuwa ng’oa viongozi a wilaya, Halmashauri na Bodi kutokana na wao kumpiga kutaka kuvunja mkataba na EBN.
Katibu wa Burunge WMA Benson Mwaise amekiri kuona tangazo la kutangazwa kitalu hata hivyo amesema yeye kama katibu ahusiki wala bodi ya wadhamini ambao ndio wanamamlaka kisheria kutangaza.
Afisa Uhusiano wa EBN Charles Sylvester amesema wameshtushwa na tangazo lililotolewa kwenye vyombo vya habari kuwa kitalu kipo wazi na kutaka kampuni zitume maombi wakati wao wapo bado na wamekuwa katika Kitalu hicho zaidi ya miaka 10 sasa.
“Tumeuliza WMA tumeelezwa ni uamuzi wa spika na tayari Bodi ya wadhamini ambao ndio wana mamlaka ya kutangaza kitalu imekana kuhusika na tangazo hilo,” amesema.
Amesema kwa zaidi ya miezi mitatu kumekuwepo na mgogoro ndani ya WMA kutokana na spika ambaye anatumiwa na kampuni Moja ya uwindaji kutaka kuvunja mkataba bila kufuata taratibu lakini pia kudaiwa kushawishi viongozi wengine WMA.
Amesema kampuni Yao ambayo imewekeza katika eneo hilo imekuwa na manufaa makubwa kwa jamii ikiwepo ujenzi wa shule, kutoa usafiri wanafunzi,kutoa fedha vikundi vya wanawake, kufundisha ujasirimali na inatumia zaidi ya sh 400 kila mwaka kupambana na ujangili kwa kishirikiana na WMA, Mamlaka ya usimamizi Wanyamapori TAWA na hifadhi ya Tarangire.
Burunge WMA ina eneo la kilomita za mraba 283 ambapo kuna wawekezaji kadhaa wa utalii na EBN ndio mwekezaji mkubwa ambaye ametoa ajira kwa zaidi ya watu 200 kutokana na kuendesha shughuli za Utalii wa picha na kambi za Utalii na amekuwa na program za kupambana na ujangili.