Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi akizungumza
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi
Na Deogratius Temba
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umewakutanisha washiriki 30,
wawakilishi wa mashirika na vikundi kutoka mikoa tisa ya mradi wa Ujenzi wa
TAPO la Ukombozi wa wanawake na
uimarishaji wa harakati za kupigania Haki za wanawake na usawa wa Kijinsia
nchini Tanzania.
Mradi huu unaojulikana kama
“Sauti za Wanawake na Uongozi” unaofadhiliwa na Ubalozi wa Canada (GAC)
unalenga kuhakikisha kila mwanajamii anatambua umuhimu wa haki za wanawake,
usawa wa Kijinsia na kusimamia misingi ya Haki na Usawa wa Kijinsia katika
utendaji wa kila siku katika jamii.
Warsha ya siku mbili (2)
inayofanyika katika Ofisi za TGNP, imejikita katika kuvuna matokeo ya
mafunzo ya ufeminia waliyopatiwa hapo awali kwa lengo la kutambua michango ya
mashirika mbalimbali na vikundi katika kuendeleza na kuimarisha vuguvugu la
utetezi wa haki za wanawake.Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, Mkurugenzi
Mtendaji wa TGNP, Lilian Liundi, amesema kwamba mradi huo unalenga kuhakikisha
vuguvugu la harakati za kutetea Haki za wanawake na usawa wa Kijinsia
linasambaa, ili jamii yote izingatie
msingi ya usawa wa kijinsia.
“Tunatamani kuona kila mtu katika taifa letu akiwa na uelewa
wa masuala ya usawa wa kijinsia na kuhsehimu haki za binadamu. Nyie ambao
mnatokea kwenye taasisi na vikundi mbalimbali katika ngazi ya jamii, ndio
mmepewa jukumu la kusambaza hii elimu na kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu
usawa wa Kijinsia na Haki za wanawake. Tunategemea kuona mabadiliko makubwa
sana huko mlinakotokea” alisema Liundi