Na. Jacob Kasiri – Ruaha
Msafara wa watalii wa ndani wapatao 500 wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe. Halima Dendegu wametembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha iliyoko mkoani Iringa hivi karibuni kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani na kuvutia wawekezaji ili wawekeze katika miundombinu ya utalii.
Akiwa katika hifadhi hiyo yenye ukubwa wa Kilometa za Mraba 20,226 mkuu wa mkoa huyo amesema, “mtalii anapokuja Hifadhi ya Taifa Ruaha ategemee kuona mandhari nzuri, wanyama wengi wazuri na wa kuvutia wakiwa katika makundi makubwa. Nilikuwa na wasiwasi leo kutomuona Simba lakini imekuwa kama ‘surprise’ mwishoni tumemuona kwa ukaribu zaidi na hizo ndizo sifa za hifadhi hii.”
“Mbali na kuona wanyama kwa ukaribu na wakiwa katika makundi yao ya asili, pia nimefarijika sana kuona watanzania wengi wamejitokeza kuja kutembelea hifadhi. Niwahakikishie tu kuwa kwetu sisi kama mkoa tutakuwa na utalii endelevu na utalii huu wa ndani tulioufanya leo katika ni mwanzo tu” aliongeza Dendegu.
Ziara ya watanzania hao kutembelea Hifadhi ya Taifa Ruaha imechagizwa kwa kiasi kikubwa na uhamasishaji wa utalii unaoendelea katika Maonesho ya “Utalii Karibu Kusini 2022” yanayoendelea mjini Iringa. Maonesho hayo yaliyoanza Novemba 09 na yanatarajia kutamatika kesho Novemba 13, 2022.