********************
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawasaka watu wanaotuhumiwa kufukua kaburi na kuchukua baadhi ya viungo vya mwili wa marehemu. Ni kwamba Novemba 05, 2022 NEEMA ENOCK MLOMBA [26] Mkazi wa Kijiji cha Kilasi – Luteba Wilaya ya Rungwe alifariki dunia muda mfupi baada ya kujifungua mtoto wa kiume katika Hospitali ya Wazazi – Meta Jijini Mbeya na baadae Novemba 06, 2022 taratibu za mazishi zilifanyika na kuzikwa katika makaburi ya Kamasulu – Mpunguti Kijiji cha Kilasi Halmashauri ya Busokelo.
Novemba 07, 2022 majira ya asubuhi ndugu wa marehemu waligundua kuwa kaburi lake limefukuliwa na mtu/watu wasiojulikana hivyo Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Daktari wa Hospitali ya Kandete tulifika makaburini na kuuchunguza mwili wa marehemu uliokuwa umezikwa katika kaburi hilo.
Katika uchunguzi ilibainika kuwa baadhi ya viungo vya marehemu ambavyo ni titi la kulia limekatwa, jicho la kulia limenyofolewa, tumbo limechanwa katikati, ulimi umekatwa na moyo umenyofolewa. Chanzo cha tukio hili ni imani za kushirikiana.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya tunalaani tukio hili na tunaendelea na misako ya nguvu kuwatafuta watu waliohusika katika tukio hili. Aidha tunatoa wito kwa mwananchi yeyote ambaye ana taarifa atoe kwa siri ili tuweze kuzifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuwabaini na kuwakamata wote waliohusika katika tukio hili. Pia nitoe rai kwa wananchi kuacha imani potofu za kishirikina kwani hazina faida kwa jamii ila zinasababisha madhara kwa jamii.