![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2022/11/IMG-20221028-WA0305-2.jpg)
Mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania (UWT) Wilaya ya Simanjiro, Mkoani Manyara, Anna Shinini (katikati) akisalimiana na wanawake waliompokea kama malkia kwa kumtandikia kanga akanyage kwenye kikao cha Baraza la UWT la Wilaya hiyo.
……………………………………….
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT) Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Anna Shinini amesema ana deni kubwa ya kuwatumikia wanawake wa wilaya hiyo waliomchagua kwa kura nyingi hivi karibuni.
Shinini ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza la wanawake wa UWT wa wilaya hiyo kilichofanyika mji mdogo wa Orkesumet.
Amesema uchaguzi umeshafanyika hivyo hakuna kambi tena baada ya kuchaguliwa kuwaongoza wanawake hao anahitaji kuwalipa utumishi uliotukuka kwani wamempa heshima kubwa mno.
Amesema ana malengo makubwa ya kutumikia jumuiya hiyo akishirikiana na wanawake wote hivyo wanapaswa kujifunga mikanda katika kutumikia nafasi walizoziomba.
“Twendeni wote kwa pamoja na tukisema tukimbie tunapaswa kukimbia wote na tukisema tusimame basi tusimame wote ila atakayebaki nyuma tutamuacha,” amesema Shinini.
Amesema hivi sasa wanawake wamepata moyo wa kuwatumikia wananchi kwani Rais Samia Suluhu Hassan ni mwanamke hivyo wanapaswa kwenda naye sambamba.
“Hivi sasa tupo juu kupitia Rais Samia hivyo tusimwangushe na kumshusha chini tumuunge mkono kwa kutimiza wajibu wetu ipasavyo,” amesema Shinini.
Amesema atawatumikia wanawake wa Simanjiro kwani ameshaacha alama kwa wasichana kwa kuwasomesha ambapo hivi sasa ni wasomi wakiwemo madaktari na wanasheria.
Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Manyara, Regina Ndege amempongeza Shinini kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UWT wilaya ya Simanjiro.
“Ninakupongeza mno Mwenyekiti mpya kwa kuchaguliwa kushika nafasi hii, wanawake wa Simanjiro wamekupa heshima kubwa hivyo usiwaangushe shirikiana nao kwa bidii zote,” amesema Ndege.
Mwenyekiti wa madiwani wa viti maalum wa wilaya ya Simanjiro, Bahati Partison amesema Shinini ni hazina ya uongozi hivyo wanawake wanapaswa kumpa ushirikiano wa kutosha.
“Miaka ya nyuma nilipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa UWT wa Wilaya ya Simanjiro, kipindi hicho kati ya nafasi tatu nilizokuwa nazo moja nilimchagua Shinini kuwa mjumbe wa kamati ya utekelezaji,” amesema Bahati.