Mafundi kutoka kampuni ya Dar es Salaam Maritime Group wakiendelea kufanya ukarabati wa kivuko cha MV. TANGA katika eneo la Pangani Mkoani Tanga, Kivuko cha MV. TANGA kinatarajiwa kurejea kuanza kutoa huduma mwishoni mwa mwezi huu katika eneo la Pangani na Bweni Tanga.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro N.Kilahala akishuka kutoka kwenye kivuko cha MV. TANGA mara baada ya kumaliza kukikagua hapo jana, kivuko hicho kinafanyiwa ukarabati mkubwa na kampuni ya Dar es Salaam Maritime Group katika eneo la Pangani Mkoani Tanga, Kivuko cha MV. TANGA kinatarajiwa kurejea kuanza kutoa huduma mwishoni mwa mwezi huu katika eneo la Pangani na Bweni Tanga. Nyuma yake ni Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Bi. Josephine Matiro.
Picha ni kivuko cha MV.PANGANI II kikielea majini kutokea eneo la Bweni kuelelekea eneo la Pangani jana kikiwa na abiria. Kivuko hicho kwa sasa kinatoa huduma katika eneo hilo kufuatia kivuko cha MV. TANGA kupelekwa kwenye ukarabati mkubwa ambao unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro N.Kilahala katikati akitoa maagizo kwa mkandarasi kutoka kampuni ya Dar es Salaam Maritime Group Mhandisi Michael Wilson (wa pili kulia) wakati akikagua maendeleo ya ukarabati wa kivuko cha MV. TANGA unaoendelea katika eneo la Pangani Mkoani Tanga jana. Kutoka Kulia ni Meneja wa TEMESA Tanga Mhandisi Jairo Nkoroka, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi TEMESA Bi. Josephine Matiro na wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Kivuko cha Pangani Mhandisi Abdulrahman Ameir.
PICHA ZOTE NA ALFRED MGWENO (TEMESA TANGA)
………………………………..
(Na. Alfred Mgweno TEMESA Tanga)
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA) Lazaro N. Kilahala, Tarehe 7 Novemba 2022, amekagua ukarabati unaoendelea wa kivuko cha MV.TANGA kinachofanyiwa ukarabati mkubwa katika eneo la Pangani Mkoani Tanga na kumuagiza mkandarasi kuhakikisha anamaliza ukarabati huo haraka iwezekanavyo ili kivuko hicho kirejee kutoa huduma katika eneo hilo.
Kilahala amekagua ukarabati wa kivuko hicho akiambatana na Meneja wa TEMESA Tanga Mhandisi Jairos Nkoroka Pamoja na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi Bi. Josephine Matiro, Mkurugenzi wa Matengenezo na Huduma za Ufundi Mhandisi Hassan Karonda na Mkuu wa Kivuko cha Pangani Bweni Mhandisi Abdulrahman Ameir.
Mkandarasi, Kampuni ya Dar es Salaam Maritime Group inayosimamia ukarabati wa kivuko hicho Mhandisi Michael Wlson aliahidi kumaliza ukarabati huo ndani ya mwezi huu wa Novemba.
Awali Mtendaji Mkuu alitembelea karakana ya Mkoa wa Tanga na kuzungumza na watumishi ambapo aliwaagiza kubadili namna wanavyofikiri kwani miongoni mwa mabadiliko makubwa kabisa yanayotakiwa kutokea TEMESA, badiliko kubwa ni namna ya kufikiri kibiashara zaidi.
Kilahala amesema sehemu kubwa ya tatizo la TEMESA ilikuwa ni kutokutambua kwamba kuna tatizo hivyo akaupongeza uongozi wa Mkoa huo chini ya Meneja wa Mkoa Mhandisi Jairos Nkoroka kwa kutambua kwamba kuna tatizo na kuonyesha ari ya kutatua matatizo yaliyopo huku akiwasisitizia kubadili mitazamo ya utendaji kazi na kutatua yale ambayo yamekuwa yakilalamikiwa siku zote.
”Niwape changamoto menejimenti yenu, mjielekeze katika namna gani kituo chenu kitaweza kujiendesha na kuwa kituo cha biashara ambacho kipo kibiashara zaidi na kinatengeneza mapato yake ya kukiwezesha kujitegemea.” Alisema Kilahala.