Na Mary Gwera, Mahakama
Mahakama ya Tanzania inaendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha kuwa inatekeleza ipasavyo jukumu lake la msingi la utoaji haki sambamba na kufikia kwa vitendo Dira yake ya Utoaji Haki Sawa kwa wote na kwa wakati.
Jitihada hizi zinadhihirishwa na kasi ya uondoshaji wa mashauri katika ngazi mbalimbali za Mahakama nchini ikiwemo Divisheni za Mahakama Kuu ya Tanzania mojawapo ikiwa ni Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi.
Katika kikao cha Watumishi wa Divisheni hiyo kilichofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Shule ya Sheria ‘Law School’ jijini Dar es Salaam, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Mgeyekwa amewapongeza watumishi wa Divisheni hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano ulioiwezesha Mahakama hiyo kuondosha jumla ya mashauri 2249 kwa kipindi cha mwezi Februari 2022 hadi Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na Watumishi wa Divisheni hiyo, Mhe. Mgeyekwa alisema kuwa idadi hiyo inajumuisha jumla ya mashauri ya mlundikano 167 yaliyovuka mwaka 2021.
“Kila mtumishi amekuwa na mchango mkubwa sana kwa sababu kazi ya kuondosha mashauri sio kwa Majaji peke yao, bali kila mtumishi. Hivyo, pongezi za takwimu nzuri za uondoshaji mashauri zinakwenda kwa kila mtumishi wa Divisheni hii,’ alisema.
Anaeleza kuwa, katika kipindi hicho cha Februari hadi Oktoba mwaka huu mashauri yaliyofunguliwa yalikuwa 1684, yaliyoamuliwa 2249 na yanayoendelea (pending) ni 1014.
Aidha; Mhe. Mgeyekwa anabainisha kuwa, hadi kufikia tarehe 04 Novemba, 2022 mashauri ya mlundikano yaliyosalia katika Divisheni hiyo ni 46 pekee huku 12 kati ya hayo yapo nje ya uwezo wa Mahakama hiyo kwa sababu kuna mashauri ya rufaa yanaendelea Mahakama ya Rufani na sababu nyingine ni kutolewa kwa amri za kutoendelea kuyasikiliza kutoka Mahakama ya Rufani. Ameongeza kuwa, “mkakati uliopo ni kumaliza mashauri 34 kabla ya mwisho wa mwaka huu.”
Jaji Mfawidhi huyo anaongeza kwamba, Divisheni ya Ardhi imefanya jitihada mbalimbali zenye lengo la kuondosha mashauri mojawapo ikiwa ni pamoja na kutumia vikao maalum vya kuendesha mashauri ‘sessions’ ambapo mashauri 59 yalipangiwa mbele ya Majaji watano (5) kutoka nje ya Kituo, kati ya hayo mashauri 51 yalimalizika, saba (7) yanaendelea kusikilizwa na shauri moja (1) linasubiri hukumu.
“Divisheni imeweka kipaumbele cha kibajeti kwenye kuondosha mashauri hasa ya mlundikano ili kufikia malengo iliyojiwekea ambapo walilazimika kualika Majaji na Naibu Wasajili kutoka vituo vingine ili kuongeza nguvu zaidi ya kuondosha mashauri hayo,” anasisitiza Jaji Mfawidhi.
“Mbinu hii yenye matokeo chanya huongeza matumizi ya bajeti, kwa kuwa mashauri ndiyo jukumu la msingi la Mahakama, Menejimenti imeona ni busara kujikita kwenye matumizi hayo, ambapo tulialika Majaji na Naibu Wasajili walioendesha vikao vya Mahakama ‘session’ na kuiwezesha Divisheni kung’ara na hivyo watumishi wote mnastahili kujipongeza na kuona fahari,” alisisitiza Mhe. Mgeyekwa.
Katika kikao hicho kilichohudhuriwa na Majaji na Watumishi wote wa Divisheni hiyo, mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo Mpango Mkakati wa Mahakama wa 2020/2021 hadi 2024/2025. Katika mada hii watumishi watatu (3) wa Divisheni hii Bw. Ukani, Mlinzi, Bi. Carolina Mambo, Msaidizi wa Kumbukumbu na Bi. Radhia Mpinga, Mwandishi Mwendesha Ofisi walifanya mawasilisho kwa umahiri mkubwa na kuonesha namna ambavyo Mpango Mkakati umeeleweka kwa watumishi wa kada zote.
Aidha, Mtaalam Mwezeshaji wa mada hii alikuwa Bw. Kisingi Mhando, Mchumi kutoka Makao Makuu ya Mahakama ambaye alitoa ufafanuzi wa kina kuhusu vipengele muhimu vya Mpango Mkakati huo na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wake.
Mada nyingine iliyowasilishwa na Mwezeshaji, Bi. Betty Jones almaarufu kama ‘BJ’ ilihusu Mbinu za Kukabiliana na Msongo wa Mawazo (Stress Management) katika maisha ya kila siku nje na mahali pa kazi ili kuwajengea watumishi uwezo na mbinu za kumudu msongo ‘stress’ na kutimiza malengo ya Taasisi.
Kadhalika, Mada nyingine iliyowasilishwa ilihusu Mpango wa Bajeti ya Divisheni, Usimamizi na Matumizi yake kwa Mwaka 2022/23 iliwasilishwa na Bw. Peter Mbaguli, Afisa Tawala akishirikiana na Bibi. Hawa Wanguvu, Afisa Hesabu Mwandamizi.
Katika majadiliano ya pamoja watumishi walitoa hoja zilizolenga kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kuongeza idadi ya watumishi, vitendea kazi, vikao vya watumishi wote pamoja na kuboresha masilahi ya watumishi ili kuwapunguzia ukali wa maisha.
Katika ufafanuzi wa hoja hizo, Mtendaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi, Bw. Anatory Kagaruki alisema kuwa masuala yote yanazingatiwa kikamilifu huku na kuongeza kuwa, uwezo na mipango ya kibajeti katika ngazi ya Taasisi na Divisheni ndiyo unaotoa dira ya namna ya kutimiza mahitaji hayo. Alifafanua kuwa ipo mipango na mikakati ya kimenejimenti ya ndani ya Divisheni na ile ya kitaasisi ya kuboresha mazingira ya kazi. Alitoa mfano wa Programu ya Kuboresha Maslahi ya Watumishi wa Mahakama inayotekelezwa na Viongozi wa Mahakama ya Tanzania wakiongozwa na Mtendaji Mkuu.
Pamoja na kuwapongeza watumishi kwa kuchapa kazi kwa bidii, Bw. Kagaruki pia aliwasihi watumishi hao kuendelea kuwa wavumilivu, kufanya kazi kwa juhudi na maarifa ili kutoa huduma kwa kiwango kinachotarajiwa na wananchi, Serikali na Viongozi wa Mahakama.
“Nichukue nafasi hii kuwapongeza Watumishi wenzangu kwa kuchapa kazi, hata hivyo tusisahau vipaumbele vyetu ambavyo ni kuendelea na matumizi ya TEHAMA, kuimarisha ushirikiano na wadau na nidhamu kwa watumishi,” alisema Bw. Kagaruki.
Kikao hicho kilichosheheni matukio mbalimbali kilihitimishwa kwa kuwapongeza na kuwakaribisha Majaji wageni walioteuliwa Mwezi Agosti 2022 na kupangiwa Divisheni ya Ardhi. Katika tukio, Jaji mpya wa Divisheni hiyo, Mhe. Kevin Mhina alizungumza kwa niaba ya Jaji mwenzake Mhe. Jaji Hemed Lusungu kuwa wanaahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na kuahidi kwamba wanaungana na Timu ya Divisheni ya Ardhi kutimiza malengo yaliyopo.
Zoezi lingine lililofanyika lilikuwa ni la utoaji wa zawadi kwa mfanyakazi bora wa Divisheni hiyo Bw. Nkotya Muro, Mlinzi ambaye alipongezwa na Jaji Mfawidhi kwa kuchaguliwa na wafanyakazi na kuwasihi watumishi wengine hasa vijana kuiga mfano huo.
Akitoa neno la kufunga kikao kwa niaba ya Jaji Mfawidhi, Jaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi, Mhe. Isaya Arufani alipongeza uongozi wa Divisheni hiyo kwa kuandaa kikao hicho na matukio yote ambayo yamewaunganisha pamoja. Akiongeza kwamba, tukio hilo limesisimua ari na morali ya watumishi wote na kwamba ufanisi na tija ya kazi itaongezeka maradufu.
Watumishi walionesha kufurahishwa na kikao hicho na kushauri vikao na matukio ya aina hiyo yafanyike mara kwa mara kwa sababu yanaimarisha umoja na upendo miongoni mwa watumishi. Mtumishi mmoja alisema kuwa kukaa pamoja na Majaji ambao ni viongozi adimu kukutana nao tena nje ya mazingira ya ofisi ni suala la kupongeza na kuendelezwa kwa kuwa inafanya watumishi kuwafahamu zaidi viongozi wao na hata kujifunza mambo mengi kutoka kwao.
Katika kuhakikisha kwamba, azma ya Mahakama ya kuongeza kasi ya usikilizaji wa Mashauri na kuondoa mlundikano, Mahakama iliweka idadi ya mashauri yanayopaswa kumalizwa na Maafisa wa Mahakama (Majaji na Mahakimu) ambapo Hakimu wa Mahakama za Mwanzo anapaswa kumaliza mashauri 260 kwa mwaka, mashauri 250 kwa Mahakama za Hakimu Mkazi na mashauri 220 kwa ngazi ya Mahakama Kuu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Mgeyekwa akizungumza na Watumishi wa Mahakama hiyo (hawapo katika picha) katika kikao cha Watumishi kilichofanyika hivi karibuni katika Ukumbi wa Shule ya Sheria ‘Law School’ jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Majaji na Watumishi wengine wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa kikao cha Watumishi kutoka kwa Jaji Mfawidhi wa Divisheni hiyo, Mhe. Agnes Mgeyekwa (hayupo katika picha).
Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Dkt. Benhajj Masoud (aliyesimama) akizungumza jambo wakati wa kikao cha Watumishi wa Divisheni hiyo. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Mgeyekwa.
Mtendaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Bw. Anatory Kagaruki akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa katika kikao cha Watumishi wa Divisheni hiyo kilichofanyika hivi karibuni. Kulia ni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Crisencia Kisongo.
Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi wakiwa katika kikao kilichofanyika hivi karibuni katika Ukumbi ya Shule ya Sheria ‘Law School of Tanzania) jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi wakifuatilia kwa makini kikao cha Watumishi wa Divisheni hiyo kilichofanyika hivi karibuni.
Mchumi kutoka Kurugenzi ya Mipango na Ufuatiliaji-Mahakama ya Tanzania, Bw. Kisingi Mhando akiwasilisha mada ya Mpango Mkakati wa Mahakama (2020/2021-2024/2025) kwa Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi (hawapo katika picha) wakati wa kikao chao kilichofanyika hivi karibuni.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi wakimsikiliza Mwezeshaji, Bi. Betty Jones (aliyesimama mbele) alipokuwa akiwasilisha mada ya Mbinu za Kukabiliana na Msongo wa Mawazo (Stress Management).