Mkurugenzi Mkazi wa SWISSAID, Betty Malaki akifuatilia mkutano wa wadau wa mbegu asili unaofanyika jijini Dodoma Ofisa Mradi wa Shirika la Kilimo Endelevu (SAT), Salma Yassin akiwasilisha mada kwa wadau wa kiliko hai na mbegu asili wanaokutana jijini Dodoma Bwana Shamba, Charles Boniventure akizungumzia umuhimu wa Kisamvu cha Chaya kama mboga yenye protini niyingi kwa washiriki wa mkutano wa wadau wa mbegu asili
Bwana Shamba kutoka ECHO East Afrika, Charles Boniventure akimuonesha,Ofisa Mradi wa Utafiti na Ushawishi wa Kilimo Hai SWISSAID, Gladness Martin kitabu chenye maelezo ya mbegu asili
***********************
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WADAU wa mbegu asili na zilizosahaulika wamekutana jijini Dodoma kwa siku tatu kujadili changamoto na kuzitafutia majibu ili mbegu hizo ziweze kutambulika kutunzwa na kuchangia katika uhakika wa upatikanaji wa chakula nchini.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Mratibu wa Shirika lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na Utunzaji wa Bioanuai Tanzania (TABIO), Abdallah Mkindi alisema wadau hao wamekutana kujadili namna ya ambayo itawezesha kilimo hai au kilimo ikolojia kinaweza kupewa msukumo hapa nchini.
Alisema kilimo hai au ikolojia kitawezesha matumizi ya mbegu asili na mazao yaliyosahaulika kupewa kipaumbele na wakulima jambo ambalo litakuza soko la mazao yao.
Mkindi alisema matumizi ya mbegu asili yatakuwa endelevu, iwapo kutakuwa na mijadala mbalimbali ambayo inashirikisha wadau wa sekta ya kilimo na mbegu.
Alisema katika siku tatu hizo wadau watajadiliana kuhusu sera na sheria zilizopo katika kusimamia sekta ya mbegu ambayo ni muhimu kwenye kupata chakula safi na salama kwa ajili ya matumizi ya watu.
“Mkutano huu umeshirikisha wadau mbalimbali kama Shirika la SWISSAID TANZANI, Alliance for Food Sovereignty in Afrika (AFSA), Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Shirika la Kuendeleza Kilimo Hai Barani Afrika (AFRONET), PELUM Tanzania na wengine, ambapo tunatarajia kutoa na maazimio yenye maslahi ya kuendeleza mbegu asili,” alisema.
Mkindi alisema iwapo wakulima watakuwa na uhakika wa mbegu asili ni wazi chakula ambacho kitazailishwa kitakuwa safi na salama katika afya ya watumiaji.
Mkurugenzi Mkaazi wa SWISSAID- Tanzania Betty Malaki, alisema shirika hilo kwa kushirikiana na wadau wangine kama mashirika ya kiraia, vikundi vya wakulima, watafiti na serikali katika kuwasaidia wakulima kutunza mbegu za asili na kuzitumia katika kuongeza uhakika na usalama wa chakula nchini.
Mkurugenzi Mkaazi huyo alisisitiza umuhimu wa kufanya kazi na wadau wengine wa mbegu za asili ili kuona namna ambavyo sekta hiyo inaenda mbele na kumkomboa mkulima.
Alisema SWISSAID, AFSA na FIBL wameshiriki mkutano huu wa wadau wa mbegu asili ili kuongeza msukumo wa matumizi wa mbegu hizo
“Tunatamani mbegu asili zitambuliwe kisera na kuzalishwa kwa wingi ambapo tunatoa rasilimali fedha, kusimamia na kutoa ushauri na kwa hapa nchini tunashirikiana na TABIO na wengine,” alisema.
Malaki alisema mipango yao ni kufikisha elimu na kujengea uwezo kuhusu mbegu asili kwa wadau wengine kama watunga sera na wabunge, ili waweze kushiriki kuhamasisha kilimo hai kwa kutumia mbegu hizo.
Mkurugenzi huyo alisema iwapo wakulima watajikita katika matumizi ya mbegu asili usalama na uhakika wa chakula na lishe bora.
Naye Program Ofisa wa AFSA, Famara Diedhiou, alisema matumizi ya mbegu asili na kuendeleza mazao yatima ni mkakati ambao utawezesha upatikanaji wa usalama wa chakula barani Afrika.
Famara alisema AFSA inafanya kazi katika nchi 15 za Afrika ambapo kumekuwepo na matokeo chanya kwa wakulima wa maeneo hayo.
“AFSA tunajikita katika maeneo matatu muhimu ambayo ni usalama wa chakula, kuongeza uzalishaji na kuhamasisha mabadiliko ya sera katika nchi ambazo tupo, ili kuhakikisha mbegu asili zinatumika kisera na kisheria,” alisema.