Mwenyekiti wa Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania (TDA),Profesa Andrew Swai,akitoa mada kuhusu ugonjwa wa kisukari kwa waandishi wa habari Kanda ya Ziwa hivi karibuni.
Wananchi na wadau wa afya wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima (hayupo pichani) wakati kitoa taarifa kwa uma kuhusu maadhimisho ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, yanayofanyika mkoani humu kitaifa.
************************
NA BALTAZAR MASHAKA
Mwaka huu kitaifa maadhimisho ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza yanafanyika mkoani Mwanza yakiwa na kauli mbiu ya Badili Mtindo wa Maisha,Boresha afya.
Takwimu za karibuni za Shirika la Afya Duniani (WHO), idadi ya vifo vinavyotokana na magonjwa yasiyoambukiza yanatajwa kuathiri figo na kusababisha watu 4,533 kupoteza sawa na asilimia 1.03 ya vifo vyote ambapo kiwango cha magonjwa ya figo ni asilimia 14.
Taasisi ya Figo ya Taifa inaonyesha gharama za kusafisha figo kwa wiki ni zaidi ya sh. milioni 4.5 ambapo kubadilisha viungo hivyo nje ya nchi kunagharimu zaidi ya sh. milioni 50.
Idadi kubwa ya watanzania watu wazima na watoto wasio na hatia wameathiriwa na magonjwa ysiyombukiza na kuwapa mateso makubwa ya ugonjwa wa moyo,kisukari,shinikizo la juu la damu, mishipa ya damu,mifumo ya hewa na neva.
Licha ya Serikali kuhangaika na kuweka mipango na mikakati ya kupambana na kudhibiti magonjwa yasiyoyakuambukiza,bado Watanzania wengi wanaathirika na kupoteza maisha kutokana na magonjwa hayo yanayosababishwa na mtindo wa maisha na ulaji wa vyakula usiofaa.
Kisababishi kikuu cha vifo vya wagonjwa hao ni figo na mishipa ya moyo kushindwa kufanya kazi au madhara yanayotokana na matatizo ya magonjwa hayo yanayochangiwa na mtindo wa maisha na ulaji vyakula usiofaa.
Pia ujenzi wa mipango endelevu ya matibabu kwa wagonjwa wa figo,moyo,kisukari,mifumo ya neva na hewa ingali changamoto nchini,ushirikiano na jitihada za pamoja katika kudhibiti,kuzuia na kutokomeza magonjwa yasiyoambukiza katika kiwango cha kimataifa zinahitajika kwa kutekeleza mambo yatakayosaidia kupunguza magonjwa hayo.
Miongoni mwa mambo hayo ni pamoja na jamii kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi, kula mlo kamili na kuepuka tabia hatarishi za unywaji pombe, dawa za kulevya na matumizi ya tumbaku.
“Magonjwa haya yameendelea kuongezeka kwa kasi,takwimu zinaeleza kuwa asilimia 71 ya vifo vyote duniani kwa mwaka 2016 vilitokana na magonjwa hayo pia magonjwa hayo huku asilimia 75 ya vifo vyote vya watu wenye umri wa miaka 30-70,” anasema Profesa Swai.
Anasema kuwa sababu za magonjwa hayo ni pamoja na ulaji usiofaa,matumizi ya vilevi,tumbaku,kutoshughulisha mwili,msongo wa mawazo na kutopata usingizi wa kutosha.
“Idadi ya Watanzania wengi hawana uelewa wa kutosha wa matatizo ya figo,uelewa huo mdogo kwa umma umesababisha wengi kushindwa kufahamu madhara makubwa katika mifumo ya mwili kama ubongo, moyo,figo, macho,mishipa ya damu na fahamu,”anasema.
Mwenyekiti huyo wa Chama cha Ugonjwa wa Kisukari anasema magonjwa yasiyoambukiza mbali na vifo yanaweza kusababisha ulemavu mfano kisukari kinaweza kusababisha mtu kupata upofu na kukatwa viungo vya mwili.
Baadhi ya viungo kushindwa kufanya kazi na kushindwa kufanya mapenzi ipasavyo huku akisisitiza kuwa wagonjwa hao ikiwemo wa kisukari kuzingatia ulaji bora wa chakula ikiwemo vyakula halisi vya wanga visivyokobolewa.
“Ubaya wa magonjwa hayo yanawakumba hata watoto,hivyo kusababisha vifo kwa watu wakiwa na umri mdogo chini ya miaka 60, pia nashauri watu wapunguze msongo wa mawazo unaosababisha kupata magonjwa yasiyoambukiza,”anasema.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya mwaka huu anasema Magonjwa Yasiyoambukizayana madhara kimaisha, kiuchumi,kiafya,kijamii na kusababisha vifo vya mapema kwa watu wengi, hivyo wataalamu wa afya watumie maadhimisho ya mwaka huu kutoa elimu na mbinu kwa wananchi kuyaepuka na kuyakabili magonjwa hayo.
“Wakati maadhimisho haya yenye kauli mbiu ya Badili Mtindo wa Maisha,Boresha Afya yanafanyika takwimu zinaonyesha ongezeko kubwa la wagonjwa kutoka watu milioni 4 mwaka 2018 hadi kufikia milioni 4.8 mwaka 2022, ongezeko hilo kubwa linaathiri afya ya mtu mmoja mmoja,jamii na uchumi,matibabu yake yanagharimu fedha nyingi,”alisema.
Malima anasema magonjwa yasiyoambukiza athari zake katika mfumo wa maisha na kiuchumi ni kubwa sababu mapato ya mtu yanatumika kugharamia matibabu (kujitibu) pia miili huathirika.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema suluhisho la ukubwa wa gharama hizo za matibabu ni kupima afya mapema na kupuuza misemo kuwa kupima ni kumchokoza Mungu,watu wasiyachukulie poa na bla bla maadhimisho hayo na mafanikio yake ni kutengeneza performance nyingine.
“Mtu anayeshindwa kuchukua tahadhari ubora wa maisha yake unakuwa katika changamoto, elimu itolewe ili wananchi wachukue hatua ya kupima mara kwa mara badala ya kusubiri hadi waugue madhara yameshakuwa makubwa,”anashauri.
Mkuu huyo wa Mkoa alieleza kuwa watu wasiofanya mazoezi na ualaji usiofaa hatari kwa afya zao na chanzo cha kupata magonjwa yasiyoambukiza kama matatizo ya moyo,shinikizo la juu la damu,mafuta mengi,kisukari,saratani na uzito uliopitiliza.
“Mabadiliko ya mtindo wa maisha usiofaa hilo ndilo tupambane nalo,mafuta mengi,ulaji usiofaa zikiwemo chips mayai,sukari,chumvi nyingi,kutokula matunda na mboga mboga kutofanya mazoezi,tumbaku,dawa za kulevya na unywaji pombe uliokithiri,hivyo kupitia maadhimisho ya mwaka huu watu wapewe tafsiri sahihi ya kufanya mazoezi ya kujenga afya,”anasema.
Kwa takwimu anasema magonjwa yasiyoambukiza yanachangia vifo vya watu milioni 41 kila mwaka ulimwenguni sawa na asilimia 75 ya vifo vyote hivyo anashauri watalaamu wa Wizaya ya Afya kutumia maadhimisho ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza,kuwaelimisha wananchi mbinu za kuyaepuka na kuyakabili magonjwa hayo tishio kutokana na kuongezeka kwa kasi.
Meneja wa Mradi wa Shirikisho la Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA) Dr.Happy Nchimbi alisema wakati maadhimisho ya kitaifa ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza yanafanyika takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha magonjwa hayo yanaongezeka duniani kote na kuathiri nyanja zote kimaisha, kiuchumi, kiafya na kijamii.