Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa ameagiza walalamikaji wa fidia Mgodi wa North Mara ambao ni wamiliki wa mashimo ya dhahabu Nyabigena kuwasilisha vielelezo vilivyo na nyaraka muhimu kwa Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Mara kwa ajili ya kuhakikiwa ili kufahamu watu sahihi wanaotakiwa kulipwa.
Dkt. Kiruswa ametoa agizo hilo Novemba 6, 2022 katika ziara wilaya ya Tarime mkoani Mara wakati akizungumza na Wenyekiti wa vijiji, viongozi wa vikundi, Madiwani na Wabunge kuhusu malamikoko mbalimbali ya fidia.
Katika kikao hicho, Dkt. Kiruswa ameagiza hadi kufikia Novemba 30, 2022 kila anayedai ahakikishe anafikisha nyaraka muhimu zinazohitajika pamoja na mikataba yao kwa Afisa Madini ili kuthibitisha madai halisi.
Aidha, amemtaka Meneja Mkuu wa Mgodi wa North Mara kuwasilisha nyaraka na vielelezo vinavyoonyesha mikataba iliyopitiwa na wenyekiti wa vijiji pamoja na vikundi hivyo ili kutoa malalamiko yaliyopo kwa sasa.
Dkt. Kiruswa amesisitiza kuendelea kutolewa elimu kwa wananchi na semina kwa madiwani wa Kata husika ili kutoa uelewa kwa taratibu zinazohitajika kwa ajili ya kupata haki katika fidia.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele ameishukuru Serikali kwa kutoa maagizo yatakayokupunguza malalamiko ya wananchi wa Tarime.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Tarime, Mwita Waitara amesema viongozi hao wanapaswa kuungana wao kwa wao ili waweze kulipwa madai yao. Aidha, amewataka kupeleka madai husika kama ilivyoelekezwa ili haki iweze kutendeka.
Pia, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Agnes Marwa amewataka wananchi kuthamini wawekezaji. Amesema wawekezaji ni baraka katika maendeleo ya Mkoa wa Mara hususan katika Sekta ya Madini.
Aidha, Meneja wa Mgodi wa North Mara, Apolinary Lyambiko ameahidi kutoa ushirikiano kwa wananchi katika kipindi chote ili malalamiko hayo yaishe na kupisha uzalishaji uendelee katika maeneo yote yenye changamoto.
Akielezea utekelezaji wa maagizo ya Naibu Waziri, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mara Mhandisi Joseph Kumburu tayari ameshateua Afisa wa kupokea taarifa hizo katika kituo kidogo cha kuuza madini Nyamongo na kuwataka wamiliki wote wa madai ya fidia kuwasilisha taarifa zao katika kituo hicho kuanzia tarehe 7/11/2022 Saa 3 Asubuhi.