***********************
Na. WAF- DODOMA
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya imebainisha mikakati inayoendelea kuchukua katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma za dawa, vifaa na vifaa tiba unakuwepo ili wananchi wanaohitaji wanufaike na huduma hizo.
Mikakati hiyo imebainishwa leo Novemba 5, 2022 na Naibu Waziri wa Afya Mhe. Godwin Mollel akimwakilisha Waziri wa Afya katika Bunge la 9, kikao cha 5, Jijini Dodoma.
Akieleza mikakati hiyo Dkt. Mollel amesema, robo ya kwanza mwaka huu ( 2022/2023) Serikali inaendelea kutoa kiasi cha shilingi Bilioni 74 za ununuzi wa bidhaa za afya na usambazaji wake.
Amesema, katika kuimarisha uwezo wa MSD kiutendaji Serikali imeendelea kulipa deni lake kwa kiasi cha shilingi bilioni 57 ili kuhakikisha MSD wananunua bidhaa za afya na wananchi kuendelea kunufaika na bidhaa hizo pindi wanapokuwa na uhitaji.
“Serikali inaendelea kutoa fedha (TZS 74 Bilioni kwa robo ya kwanza mwaka 2022/2023) za ununuzi wa bidhaa za afya na usambazaji wake. Serikali katika kuimarisha uwezo wa MSD kiutendaji imeendelea kulipa deni lake kwa kiasi cha shilingi bilioni 57. Yote ni kuhakikisha MSD wananunua bidhaa za afya.” Amesema Dkt. Mollel
Aidha, Dkt. Mollel amesema kuwa Serikali itaendelea kufanya mabadiliko ya mara kwa mara ya watendaji ndani ya MSD kwa lengo la kuongeza tija ya shirika ambapo kwa sasa Menejimenti yote imebadilishwa pamoja na kuteua bodi mpya, huku akisisitiza muundo wa Taasisi hiyo unafanyiwa mapitio ili kuboresha utendaji.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amesema Serikali imeingia mikataba ya muda mrefu na wazalishaji wa bidhaa za afya ili kuweza kuharakisha upatikanaji wa dawa kulingana na mahitaji.
Ambapo Jumla ya mikataba 176 imeingiwa kwa ajili ya bidhaa aina 1,152 zikiwemo bidhaa za kipaumbele na tayari baadhi ya mikataba imeanza kuleta bidhaa.
Pia, amesema Bohari ya Dawa imewekewa vigezo vya upimaji wa ufanisi katika mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya ambapo kiashiria cha uwepo wa bidhaa za afya kimeboreshwa kutoka bidhaa toshelevu za mwezi mmoja hadi miezi minne kupima kiwango cha chini cha bidhaa za afya 290 ashiria ili kuhakikisha bidhaa hizo zinakuwepo wakati wote.
Kwa upande mwingine Dkt. Mollel amesema, Sambamba na kuboresha upatikanaji wa huduma za dawa, Serikali imeendelea kuboresha mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, ikiwa ni mkakati mwingine wa kuboresha huduma za afya kwa wananchi kwa gharama nafuu.
Amesema Mfuko umeendelea kufanya uraghibishaji kwa watoa huduma nchini wakiwemo vituo vya kutolea huduma vya Serikali katika kufuata miongozo ya utoaji wa huduma za afya nchini ili kuepuka makosa yanayoweza kuzuilika katika kujaza fomu za bima.
Aidha, amesema Mfuko umeweka madaktari katika baadhi ya Hospitali hapa nchini lengo likiwa ni kutoa elimu na kuchakata madai katika vituo hivyo kabla hayajawasilishwa ili kuondoa makosa yanayosababisha makato.
Mpaka sasa, Mfuko umeweka madaktari katika vituo 20 vya ngazi ya Taifa, Kanda na Mikoa kwa hospitali za Serikali/binafsi kati ya vituo hamsini vya ngazi hizo kwa kufanya hivi makato kwa watoa huduma yamepungua kwa wastani wa 4%.