Na. OMM Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga ameelekeza halmashauri zote mkoani humo kuandaa maadhimisho ya wiki ya utoaji elimu ya lishe bora katika ngazi za vijiji ili kukabiliana na tatizo la udumavu.
Ametoa kauli hiyo leo (Novemba 04, 2022) mjini Sumbawanga wakati wa hafla ya kukabidhi pikipiki Kumi na Mbili (12) kwa maafisa lishe wa halmashauri zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la udumavu ambao kwa Rukwa upo asilimia 47.9 kwa takwimu za mwaka 2018.
Sendiga alibainisha kuwa maadhimisho hayo yakifanyika itakuwa jukwaa zuri la wataalam wa lishe kutoa elimu ya uandaaji vyakula bora na ulaji sahihi kwa kutumia vyakula vinavyopatikana kwenye mazingira ya Rukwa kwa kuwa mkoa huo ni mzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula.
Akitoa taarifa ya vifaa hivyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Ibrahim Isaack alisema jumla ya pikipiki Kumi na Mbili zimetolewa kwa Halmashauri za Kalambo (4), Sumbawanga Vijijini (3), Nkasi (3) na Manispaa ya Sumbawanga (2).
Dkt. Ibrahim alisema pikipiki hizo zitakwenda kufanya kazi ya elimu ya lishe, kuboresha utoaji chanjo na kufuatilia magonjwa ya milipuko vijijini.