WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni akizungumza na wajumbe wa Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza (SHIMA) kabla ya kuizindua Bodi hiyo leo Novemba 3, 2022, jijini Dar es Salaam. Ameitaka Bodi hiyo kuwa na maono na kujiendesha kibiashara ili kutimiza malengo ya Serikali. Kulia ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Maduhu Kazi. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi, Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, Saidi Mwema. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni (katikati meza kuu) akimsikiliza Afisa Mtendaji Mkuu na Katibu wa Bodi ya Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza (SHIMA), Muremi Marwa, katika Kikao cha Uzinduzi wa Bodi hiyo, leo Novemba 3, 2022, jijini Dar es Salaam. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
************************
Na Mwandishi Wetu, MoHA, DSM.
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni ameitaka Bodi mpya ya Shirika la Uzalishaji Mali la Magereza (SHIMA) kuwa na maono na kujiendesha kibiashara ili kutimiza azma ya Serikali.
Akizungumza wakati akiizindua Bodi hiyo jijini Dar es Salaam leo Novemba 3, 2022, alisema Bodi hiyo ikiwa na maono ya kibiashara itatekeleza azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ambapo moja ya kipaumbele chake ni kuboresha Jeshi na mifumo yake.
Masauni alisema katika kutekeleza mipango hiyo, Rais aliongeza Bajeti ya jeshi hilo, ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ipasavyo kwa ufanisi na weledi.
Alisema kutoka na wajumbe wa bodi hiyo aliowateua kwa sifa na weledi wao, serikali ina matumaini makubwa kuwa watatekeleza majukumu yao kwa uzalendo wa kusaidia Taifa katika Jeshi la Magereza kusonga mbele zaidi.
“Ndugu wajumbe, lengo kuu la SHIMA ni kusaidia Jeshi la Magereza kutenganisha majukumu ya kijeshi na biashara bila muingiliano wowote, ili kuwepo kwa mafanikio makubwa yakujiendesha na kuchangia pato la Taifa, hivyo ni matumaini yangu makubwa kuwa bodi hii itasaidia shirika hili kutimiza malengo hayo na kusonga mbele zaidi,” alisema Masauni.
Aidha, Waziri Masauni pia aliitaka Bodi hiyo aliyoizindua kutatua changamoto zilizopo, ambazo ni nikutokuwepo mfumo maalumu wa kujiendesha, kutozingatia kanuni na taratibu, kutokuwa na maono na nia ya dhati ya kujiendesha kibiashara na kutatua baadhi ya migogoro iliyopo.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Maduhu Kazi alisema watashirikiana kwa pamoja na Bodi hiyo, ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yake kwa mafanikio makubwa yaliyokusudiwa na Shirika hilo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi hiyo, ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, Saidi Mwema alimshukuru Waziri Masauni kwa kuwaamini na kuwateua kuongoza bodi hiyo na kumuahidi kufanya kazi kwa ufanisi kufanikisha malengo ya Bodi hiyo.
Alisema wanatekeleza maagizo yote aliyowapa kwa ushirikiano, ili kutimiza maono ya kuanzishwa kwa Shirika hilo.
Alisema watahakikisha wanatekeleza shughuli zao kwa weledi, kufuata sheria na kushirikiana na uongozi wa SHIMA na kuendeleza yale yote yaliyofanyika katika uongozi uliopita.
“Mheshimiwa Waziri kwa maelezo uliyotoa tunajukumu kubwa sisi viongozi na wajumbe wote kuhakikisha tunasaidi serikali yetu na taifa kwa ujumla kupitia Bodi na Shirika hili,” alisema Mwema.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu na Katibu wa Bodi ya Shirika hilo, Muremi Marwa alisema shirika hilo linamiradi 24 ambapo tisa inahusika na viwanda vya sabuni na ushonaji, na 15 vinahusika na kilimo na ufugaji.
Bodi hiyo iliyozinduliwa leo Wajumbe waliteuliwa hivi karibu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na leo baada ya kuzinduliwa imekutana kwa mara ya kwanza na kuweka mikakati ya kiutendaji katika kufanikisha malengo ya Shirika hilo.