*********************
Na. WAF – Mwanza
Waandishi wa habari wa Mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Geita, Kagera, Mara na Mwanza wamepewa mafunzo juu ya uelewa wa kujikinga pamoja na namna ya utoaji wa taarifa za Magonjwa Yasiyoambukiza.
Mafunzo hayo yametolewa leo Novemba 2, 2022 Jijini Mwanza na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Chama cha Kisukari Tanzania (TDA) na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA).
Mwenyekiti wa Chama cha Kisukari Tanzania (TDA) Prof. Andrew Swai amebainisha kwamba miongoni mwa sababu za kupata Magonjwa hayo ni pamoja na kukosa Usingizi wa Kutosha, kutokufanya mazoezi na kula vyakula bila mpangilio.
“Ili tuepukane na Magonjwa haya yasiyoambukiza tunapaswa kufanya mazoezi angalau kwa siku mara moja, kupata muda mzuri wa kulala kuanzia saa Saba hadi Nane pamoja na kupunguza kuwa na Msongo wa mawazo ambao unasababisha kupata Magonjwa kama Saratani.” Amesema Prof. Swai
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo waandishi wa habari ya mikoa hiyo ili kuweza kutoa taarifa na ujumbe sahii kwa wananchi wa mikoa hiyo ili kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza nchini.