KAMISHNA wa Maadili, Jaji wa Rufani Sivangilwa Mwangesi, akizungumza na waandishi wa habari loe Novemba 2,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu kuanza kuhakiki mali za viongozi wa umma.
……………………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
OFISI ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma,inatarajia kuanza uhakiki wa rasilimali, maslahi na madeni kwa viongozi wa umma 658 watahakikiwa.
Hayo yamesewa leo Novemba 2,2022 jijini Dodoma na Kamishna wa Maadili, Jaji wa Rufani Sivangilwa Mwangesi, amesema kuwa kazi ya uhakiki itaanza Novemba 7 hadi 18, mwaka huu.
Jaji Mwangesi amesema kuwa viongozi watakaohakikiwa ni pamoja na Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Majaji na Makatibu Wakuu na watakaobainika kuwa na kasoro watafikishwa kwenye Baraza la Maadili.
“Viongozi watakaohakikiwa ni baadhi ya Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na wengine wa kada mbalimbali. Uhakiki utafanyika kwenye Mikoa 10 ya Kilimanjaro, Dar es salaam, Lindi, Njombe, Dodoma, Tanga, Geita, Mwanza, Tabora na Iringa,”amesema Jaji Mwangesi
Amewataka viongozi wanaofanyiwa uhakiki kufanya maandalizi kwa mujibu wa maelekezo yaliyotolewa huku wito ukitolewa kwa wananchi wenye taarifa muhimu kuhusu rasilimali na madeni ya viongozi kutoa ushirikiano.
”Wananchi wenye taarifa muhimu kuhusu rasilimali na madeni ya viongozi wanatakiwa kutoa ushirikiano ili kufanikisha zoezi hilo”amesema
Aidha amewaomba Wakuu wa Mikoa, Makamanda wa polisi na mamlaka nyingine kutoa ushirikiano kwa maafisa watakaofika kwenye maeneo hayo ili kufanikisha uhakiki huo.
“Nitoe tahadhari kwa viongozi wahusika wajihusishe na watu watakaokuja na vitambulisho vya kuonesha hao ndio wahusika wa sekretarieti ili wasiangukie kwenye mikono ya matapeli ambao huingilia mchakato huo,”amesema
Pia amewakumbusha viongozi wote ambao wanapaswa kutoa matamko yao ya rasilimali, maslahi na madeni ya mwaka 2022 kutimiza takwa hilo la kisheria.
“Matamko ya viongozi yameanza kupokelewa kuanzia mwezi Oktoba na tarehe ya mwisho ni Desemba 31, mwaka huu,”amesema
Naye Katibu wa Idara ya Usimamizi wa Maadili, John Kaole, amesema kuwa kwa mwaka 2021 ulifanyika uhakiki kwa viongozi 425 ambapo 36 walibainika kuwa na kasoro kwenye masuala ya mali na mgongano wa maslahi.
“Hatua zilizochukuliwa kuna ambao wamepelekwa kwenye uchunguzi na hatimaye kwenye baraza la maadili lakini kuna wengine kasoro zao zilikuwa zinarekebishika walipewa ushauri wa kurekebisha,”amesema