Serikali imesema katika kutekeleza maboresho ya mazingira ya Biashara hapa Nchini Imeanzisha kitengo maalumu kinachoitwa Business Inviroment Unit (BIU) ambacho kitasimamia sekta zote za kibiashara ili kubainisha Changamoto na kero zilizopo katika Biashara na kuzifanyia utatuzi kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali zikiwemo za kisera na mamlaka za kodi.
Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya semina na kamati ya kudumu ya bunge ya Viwanda,Biashara na Mazingira Bungeni Dodoma , Naibu waziri Wizara ya Uwekezaji , Viwanda na Biashara Mh. Exaud Kigahe amesema kuwa mpango huo unaojulikana kama Blueprint utajikita kusimamia changamoto zote katika sekta mbalimbali zinazolalamikiwa Wafanyabiashara kuwa mazingira magumu katika Uwekezaji na ulipaji kodi na tozo mbalimbali.
Exaud amesema kuwa mpango huo ulianza mwaka 2019 baada ya kubaini wafanyabiashara wengi kutoka sekta mbalimbali kukumbana na changamoto nyingi ambazo zinakwamisha kazi zao licha ya kwamba utekelezaji wake ulikuwa haujaanza.
“Kama mnavyojua kwa tafiti za mwaka 2020 katika mataifa tuko namba 141 ambayo sio nzuri hivyo tukaona kupitia mfumo huo wa kuboresha mazingira na ufanyaji biashara Nchini kuona namna ya kuondoa vikwazo kwenye sekta zote hasa wingi wa tozo ambazo sio za lazima hususani kwenye usafirishaji, kilimo , nishati,maji, mafuta ambapo kitengo hiki kitaratibu na kuzielekeza kutatua changamoto,” amesema Exaud Naibu Waziri Wizara ya Uwekezaji , Viwanda na Biashara.
Amesema vikwazo vingine ni kulikuwa na utitiri wa taasisi za udhibiti na muingiliano wa majukumu yao hasa TBS na TFDA hivyo kupitia Blueprint ikawa na jukumu la kubaini changamoto zote kutoka kwa wadau na kuzifanyia kazi .
“Leo wabunge wamepata nafasi ya kusikiliza nini tumefanya kitengo hicho ambacho kimewasilisha taarifa ya mwanzo ya mwaka wa kwanza wa kutekeleza kutatua changamoto nyingi na tayari kitengo kimeisha kuwa na bajeti yao katika utendaji kazi zao na wabunge wetu wametoa maoni yao ya namna ya kuboresha. “Amesema Exaud.
Akizungumzia manufaa yatakayopatikana kupitia mfumo huo ni pamoja na kusaidia usajili nankuanzisha biashara ndani ya siku saba kwa mfanyabiashara, kusaidia kuondoa utitiri wa kodi kutoka kwenye taasisi mbalimbali ambazo hazina tija ambazo zimepelekea wengi kufunga biashara bila faida.
Mbunge wa jimbo la Ndanda David Mwambe ni miongoni mwa wabunge waliopata semina hiyo amesema kuwa mfumo huo utakuwa na tija kwa Taifa hasa kuwasaidia wafanyabiashara kuondoa vikwazo.
Amesema licha ta jitihada zilizofanya kuna haja ya kukaa na wawekezaji wa viwanda kuongea nao namna ya kupunguza gharama za uzalishaji ambazo urudishwa kwa wananchi.