MBUNGE wa Singida Mashariki (CCM), Miraji Mtaturu, ametahadharisha kanuni zitakazotungwa kwenye muswada wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi wa mwaka 2022 kuhakikisha zinaendana na sheria ili zisiibue malalamiko kwa wananchi.
Akichangia leo bungeni, Mtaturu amesema sheria hiyo ni nzuri lakini utungaji wa kanuni hizo uendane na sheria iliyopitishwa.
“Pamoja na sheria hii kuwa nzuri na tumekuwa tukipitisha hapa, kumekuwa na changamoto ya kanuni, niombe sana kwenye eneo hili na sisi tunamuamini Waziri, sheria ikitungwa nzuri iende hivyo hivyo na kanuni ziwe nzuri,”amesema.
Mtaturu amesema eneo la utungaji wa kanuni linaweza kuwa mwiba mwingine katika utekelezaji wa sheria zinazopitishwa na bunge.
“Tumekuwa tukipitisha baadhi ya sheria lakini ile nafasi ya kutengeneza kanuni huwa inakwenda kuharibu kabisa sheria, matokeo yake wabunge tunaulizwa mlipitishaji sheria hii, kumbe kanuni imekwenda kuharibu kabisa maudhui mazima ya sheria ambayo tumepitisha hapa,”amesema.
Amemuomba Spika wa Bunge Dokta Tulia Ackson kuomba kanuni zipelekwe bungeni ili wajiridhishe kabla hazijaanza kutumika.
Kuhusu Muswada wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania wa Mwaka 2022, amesema utaongeza wawekezaji nchini na kuongeza wigo wa ajira.
“Wawekezaji wengi walikuwa wanasita kuwekeza, leo hii wamekuwa na mahitaji ya kuona dhamira ya serikali yetu katika eneo la uwekezaji, hii imejenga imani zaidi kwa wawekezaji,”amesema.
PONGEZI KWA SERIKALI.
Mtaturu ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuja na sheria hiyo.
“Hii sheria tumeisubiri kwa muda mrefu,niishukuru na kuipongeza serikali kwa usikivu wake,kwa kusikiliza kilio cha wadau na kuja na sheria hii,”amesema.