Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Ormemei Kurian Laizer amewataka wakuu wa idara wa Halmashauri hiyo kuwa na ilani ya CCM ili watekeleze wajibu wao ipadlsavyo.
Kiria ameyasema hayo wakati akitoa hotuba yake ya kwanza kwa watumishi wa Serikali, maofisa Tarafa, watendaji wa kata, vijiji na Wenyeviti wa viijiji na vitongoji.
Amesema ilani inayotekelezwa ni ya CCM hivyo itakuwa ni ajabu sana mtaalam yeyote akawa hana hicho kitabu cha ilani anayoitekeleza ni sawa na mkristo au muislamu kutokuwa na biblia au msahafu.
“Nitoe wito kwa kila mkuu wa idara ni vyema sana ilani uwe nayo mezani kwako ukijikumbusha eneo lako unalolitekeleza limeelezwaje,” amesema Kiria.
Amesema anatumia lugha rahisi na nyepesi kuwakumbusha kutimiza wajibu wa kila mmoja wao kuwa wanapodai haki yao wakumbuke kutimiza wajibu.
“Kasoro yoyote utakayoisababisha ujue unaijengea mazingira magumu CCM jambo ambalo chini ya uongozi wangu hatutakubali,” amesema Kiria na kuongeza;
“Wananchi wetu hawana shida wanahitaji kuhudimiwa vizuri na kwa wakati, tukasikilize na kutatua changamoto zao kwani wilaya yetu ni ya wafugaji, wakulima, wachimbaji na wafanyabiashara wakubwa na wafogo wote wanategemeana,”
Amesema katiba ya CCM inaeleza wazi kila baada ya miezi sita Serikali ngazi husika itawasilisha kwa chama tawala taarifa ya miradi walivyotekeleza hivyo wajiulize kama wanafanya hivyo.
“Nitumie nafasi hii kumpongeza mkuu wetu wa Wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Hassan Serera na wasaidizi wake kwani aliwasilisha utekelezaji wa ilani kipindi cha Januari hadi Desemba 2021 kwa umahiri mkubwa,” amesema Kiria.
Amesema utaratibu huo usiishie Wilayani kwani ameelekeza ufanyike ngazi ya matawi na kata na pia mfuko wa jimbo nao utolewe taarifa yake na mbunge wa Jimbo.
“Viongozi hivi sasa siasa na uchumi kwa karne ya sasa haviachani naelekeza ombeni viwanja, mashamba, kuanzisha miradi ya kiuchumi na kuiboresha ile ya zawani kila kiongozi wa chama aonyeshe fahari kuacha alama katika kipindi cha uongozi wake,” amesema Kiria.
Amesema fahari yake wamekutana viongozi pamoja ili waende pamoja kwani mtumishi kuwa mungu mtu siyo sawa na eneo la ardhi Serikali mkajitazame upya hasa kwenye Serikali za Vijiji.