Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akizungumza na Balozi wa Cuba nchini Tanzania Komredi Yordenis Despaigne Vera (kushoto) leo Novemba 2, 2022 katika Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akimkabidhi zawadi ya kinyago cha Umoja Balozi wa Cuba nchini Tanzania Komredi Yordenis Despaigne Vera (kushoto) leo Novemba 2, 2022 mara baada ya kumaliza mazungumzo katika Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba jijini Dar Es Salaam.
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo akimkabidhi zawadi ya Vitabu Balozi wa Cuba nchini Tanzania Komredi Yordenis Despaigne Vera (kushoto) leo Novemba 2, 2022 mara baada ya kumaliza mazungumzo katika Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba jijini Dar Es Salaam.
……………………………..
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama Cha Kikomunisti cha Cuba (CPC) vimekubaliana, pamoja na masuala mengine, kuzihimiza serikali wanazoziongoza katika nchi za Tanzania na Cuba, kuendelea kuimarisha ushirikiano na urafiki kupitia sekta mbalimbali zikiwemo za Kilimo, Afya na Elimu, kwa ajili ya manufaa na maendeleo ya watu wa pande hizo mbili.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika mazungumzo ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Ndugu Daniel Chongolo na Balozi wa Cuba nchini Tanzania Ndugu Yordenis Despaigne Vera, wakati balozi huyo alipofika kumtembelea Ndugu Chongolo, Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es salaam, leo Jumatano, 02 Novemba, 2022.
Katibu Mkuu Ndugu Chongolo amefafanua kuwa, Tanzania na Cuba kupitia vyama vya CCM na CPC kwa miaka 60 sasa, zimekuwa na ushirikiano na urafiki wa kihistoria, ulioasisiwa tangu wakati wa viongozi waasisi wa mataifa hayo, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Fidel Castro katika nyanja mbalimbali za maendeleo, hivyo viongozi wa sasa, kupitia vyama na serikali hizo, wanao wajibu mkubwa wa kuimarisha zaidi na kuuendeleza kwa ajili ya tija na ustawi kwa jamii za nchi hizo.
Kwa upande wake, Balozi Yordenis Despaigne Vera ameeleza kuwa ni muhimu na lazima, kwa pande hizo mbili kuendelea kufanya kufanya kazi kwa pamoja zaidi ili kuendeleza uhusiano na urafiki ulioanzishwa na waasisi hao na kujengewa misingi imara kwa miaka kupitia vyama vya CCM na CPC.