*******************
Viongozi Vijana 12 wa vyama siasa kutoka wanachama wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), wametunukiwa vyeti baada kupata mafunzo ya mzunguko wa uchaguzi na matumizi ya mitandao ya Kijamii.
Halfa ya kukabidhi vyeti hivyo imefanyika katika makazi ya Balozi wa Uholanzi, Wiebe de Boer, Dar es Salaam, jana, na kuhudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TCD, Bernadetha Kafuko pamoja na Mwakilishi wa Balozi wa Uswiz na International Republic Institute (IRI).
Vijana hao waliopatiwa vyeti hivyo ni kutoka vyama wanachama wa TCD ni CCM, CUF, ACT-Wazalendo na NCCR-Mageuzi, ambapo Mkurugenzi wa kituo hicho, Bernadetha Kafuko, alishukuru Ubalozi wa Uholanzi kwa kusaidia TCD kuwezesha kutekeleza mradi wa vijana katika vyama vya siasa.
Katika taarifa yake Bernadetha, amesema wamefanikiwa kutoa mafunzo hayo katika Mikoa mitano ambayo ni Unguja Mjini Magharibi, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa na Kilimanjaro.
Amesema mafunzo hayo yalienda vizuri na vijana wamejifunza mambo mengi ambayo wanayafanyia kazi katika vyama vyao na wameahidi kuendelea kuyafanyia kazi kwa kufundisha vijana wengine kwenye vyama vyao.
Kwa upande wa Balozi wa Uholanzi, Wiebe de Boer, amewakaribisha vijana kwa kuitikia wito wa kumshirikisha jinsi programu ya mafunzo ilivyofanyika na namna wanavyoona imeweza na itaweza kuwasaidia katika vyama vyao.
Pia Balozi Wiebe de Boer, ameipongeza TCD kwa kutekeleza mradi wa vijana katika vyama vya siasa kwa namna ambayo wao walioenda kuona vijana wanashirikishwa katika siasa na uchaguzi.