TIMU ya watoto ya Mgusu Machinjioni wakifurahia ushindi baada ya kutwaa taji la GGML- Toto Cup kwa kuifunga timu ya Elimu Uwangani kwa jumla ya mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika Nyakabale wilayani Geita mkoani Geita. Waliosimama nyuma ni baadhi ya viongozi wa GGML wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Terry Strong.
………………………………
NA MWANDISHI WETU, GEITA
TIMU ya watoto ya Mgusu Machinjioni imefanikiwa kutwaa taji la GGML- Toto Cup baada ya kuifunga timu ya Elimu Uwangani kwa jumla ya mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliofanyika Nyakabale wilayani Geita mkoani Geita.
Mgusu Machinioni walitangazwa kuwa mabingwa wa mashindano hayo ya soka ya watoto yanayofanyika kwa kushirikisha watoto wanaozunguka migodi wa Kampuni ya Geita Gold Mining Ltd. (GGML)
GGML ambao ndio waanzilishi na waandaaji wa mashindano hayo, walizindua michuano hiyo katika kata za Mtakuja na Nyankumbu za Geita Mjini kwa lengo la kutoa elimu kwa watoto, walezi na wazazi kuhusu madhara ya kuwanyonya watoto wadogo katika shughuli za uchimbaji madini na kuwanyima fursa ya masomo.
Akizungumza katika fainali hiyo iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Terry Strong alielezea furaha yake kwa kuhudhuria katika kilele cha mashindano hayo ya kandanda kwa vijana kutoka eneo jirani la mgodi.
Alibainisha kuwa tangu kuanza kwa shughuli zao mkoani Geita, uvamizi wa watoto wadogo umekuwa ni changamoto kubwa kwenye eneo la mgodi.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa watoto ni sehemu muhimu ya jamii inayozunguka mgodi huo katika kutekeleza shughuli zao za kibiashara.
“Kama sehemu ya kujitolea kwetu kwa jamii, tumefanya uwekezaji mkubwa katika shule, hospitali na kuchangia vifaa mbalimbali vya kutoa huduma. Mathalani mwaka 2018, GGML ilijenga zaidi ya madarasa 600.
“Hii yote ni katika kuwajengea mazingira mazuri ya elimu kwa watoto wetu kwani watoto ni kizazi cha siku zijazo na ndio wanufaika wa kwanza jitihada zote tunazozifanya katika kujitolea kwetu,” alisema Strong.
Alibainisha kuwa kampuni hiyo inazingatia Kanuni Elekezi za Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Haki za Kibinadamu na Kanuni za Hiari za Usalama na Haki za Kibinadamu (VPSHR) (UNGP).
“Kwa hivyo, tumeahidi kuwalinda watoto dhidi ya hatari zozote zinazohusiana na mazoea yetu ya biashara,” alisema.
Aidha, kwa mujibu wa Strong, idadi ya watoto wanaovamia na kuingia kwenye eneo la mgodi ni jambo ambalo linachukuwa kwa tahadhari kubwa na mgodi huo.
“Kwa kawaida sisi hutumia neno “kuwaokoa watoto” badala ya “wavamizi” kwa sababu watoto wanalindwa na sheria za kitaifa na kimataifa. Hata hivyo, imefahamika kwamba idadi kubwa ya watoto waliookolewa katika eneo la mgodi wanapatikana ndani au nje ya eneo la mgodi wetu,” alisema.
Alisema kati ya mwaka 2019 na 2020, watoto 680 waliokolewa ndani na nje ya eneo la uendeshaji la GGML.
Alisema ili kukabiliana na hali hiyo, GGML imeshirikiana na serikali za mitaa kuanzisha programu kadhaa za uhamasishaji, ikiwa ni pamoja na mawasiliano ya moja kwa moja na shule za sekondari na msingi.
Strong alisema, “Katika jitihada za kuwaweka watotokuwa wachangamfu, washiriki program mbalimbali wakati wa mapumziko ya likizo na kukuza hamasa ya kuwa na afya njema, tumechagua kufadhili mashindano ya kandanda kwa ajili ya vijana waliopo ndani na nje ya eneo la mgodi.”
“Tunaamini kuwa kila shindano linapohitimishwa, wachezaji wenye vipaji vya soka wataibuka na kuchaguliwa na klabu kubwa kama Geita Gold Football Club (inayodhaminiwa na GGML) kuchuana katika uwanja wa Magogo ambao pia unadhaminiwa na GGML, lengo ni kuwaokoa hawa na kuwasaidia kukuza vipaji vyao kisoka,” alisema.