********
Na WAF- DOM.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa jamii na lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. James Kengia ametoa wito kwa wataalamu wa afya kwenda kuanzisha kliniki za magonjwa yasiyoambukiza katika vituo vyao vya kutolea huduma.
Dkt. Kengia amesema hayo wakati akifunga mafunzo ya magonjwa yasiyoambukiza yaliyoratibiwa na Wizara ya Afya, OR TAMISEMI pamoja na Wadau wa chama cha Kisukari Tanzania (TDA) kwa Watoa huduma (Madaktari, Wauguzi) pamoja na wakufunzi Jijini Dodoma.
Amesema, ni matarajio kwamba elimu iliyotolewa kwa siku tano itaenda kuwekwa kwa vitendo ili kuleta mabadiliko katika kutatua changamoto za magonjwa yasioambukiza nchini, ikiwemo namna ya kutambua na kuwahudumia wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza.
“Tutakaporudi vituoni tuhakikishe tunaanzisha kliniki za magonjwa yasiyo ya kuambukiza kwa vituo ambavyo havina na kuboresha kliniki hizo kwa maeneo ambayo zipo tayari, kazi hii ifanywe kwa ushirikiano na wauguzi ambao pia nimepata taarifa wapo waliopatiwa mafunzo haya.” Amesema.
Sambamba na hilo, amewataka kuandaa Mikakati shirikishi na Mipango shirikishi na jumuishi ya kutekeleza Afua mbalimbali za kukinga na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza, Afya ya akili na ajali katika maeneo yao ya kutolea huduma.
Aidha, amewataka kutenga fedha kwa ajili ya afua za magonjwa yasiyoambukiza, afya ya akili na ajali na kuacha tabia ya kuwategemea Wadau tu wakati wote.
Serikali imefanya maboresho makubwa katika miundombinu ya kutolea huduma za afya katika majengo, watumishi na vifaa tiba. Maboresho yaliyofanyika ni lazima yaende sambamba na ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo hivi. Amesisitiza Dkt. Kengia.
Naye, Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wakuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza Bi. Valeria Millinga amesema, moja kati ya mikakati iliyopo ni kuimarisha huduma za msingi kwa kuvijengea uwezo vituo vyote vya afya 600 kwa kuwapa mafunzo Watoa huduma angalau wanne katika kila kituo ili kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.
Mwisho.