Na Alex Sonna-DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amewataka Wananchi wa mkoa wa Dodoma kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa Jamhuri kwa ajili ya kushuhudia uzinduzi wa Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi.
Uzinduzi huo utafanyika Kesho Octoba 31,2022 na Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 30,2022 Jijini Dodoma Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa ni vyema kila Mtanzania kesho akaandika historia kwa kuhudhuria uwanjani moja kwa moja ama kufuatilia tukio hilo Mbashara kwa njia ya vyombo vya habari.
“Mimi binafsi natamani sana kujua Mkoa wangu wa Dodoma una watu wangapi na Kama vile haitoshi naamini kila mtanzania pia ana tamaa kama mimi ya kutaka kujua tupo wangapi hii ni historia kwani tunakwenda kujua ni namna gani ya kuwahudumia wote kwa usawa,
Na kuongeza kuwa “Ni lazima tujue tupo wangapi na siku yenyewe ya kujua hilo ni kesho ambapo Mheshimiwa Rais wetu ataliongoza taifa katika Uzinduzi huo,”Amesema Senyamule
Katika hatua Nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amesema katika usiku wa kuamkia siku ya tukio (Usiku wa Octoba 30,2022) majira ya saa sita usiku itarushwa Fataki kuashiria tukio hilo.