*********************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WATENDAJI wa kata na viijiji Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wametakiwa kuhakikisha lishe ni ajenda ya kudumu katika vikao vya kisheria ili kuboresha hali ya lishe na kupunguza athari za utapiamlo katika jamii.
Mkuu wa wilaya ya Simanjiro Dkt Suleiman Hassan Serera ameyasema hayo wakati akitoa maagizo ya utekelezaji vipaumbele vya lishe ngazi ya jamii.
Dkt Serera amesema watendaji hao wanapaswa kuhakikisha lishe inakuwa ajenda ya kudumu katika vikao vya kisheria vya kamati ya maendeleo ya kata.
“Mikutano hiyo itachochea na kuibua fursa za lishe, matatizo na suluhu za kutatua matatizo ya lishe yaliyopo kwenye jamii na kwenye kata,” amesema Dkt Serera.
Amesema mikutano hiyo itahakikisha mpango kazi wa lishe unajumuisha afua za chakula na lishe, afya, maji safi, usafi wa mazingira na uchangamshi kwa watoto wadogo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Samwel Warioba amezipongeza kata za Mirerani na Emboreet kwa kuongoza kwa lishe bora kwa jamii katika wilaya hiyo.
Mbunge wa Jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amesema wanawake wajawazito wanapaswa kupewa lishe bora ili afya ya mtoto iwe nzuri na uwezo bora wa kufikiri.
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Simanjiro Kiria Laizer amesema jamii inapaswa kupewa elimu ya kuhakikisha lishe inapatikana kwa wakati hasa kwa watoto.