Mbunge wa jimbo la Arusha mjini ,Mashaka Gambo akizungumza kwenye mkutano huo wa wajasiriamali jijini Arusha .
Mbunge wa jimbo la Arusha mjini ,Mashaka Gambo akitembelea moja ya banda la mjasiriamali katika mkutano huo unaofanyika jijini Arusha.
Wajasiriamali mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wakiwa katika picha ya pamoja na wadau pamoja na mbunge wa jimbo la Arusha mjini,Mashaka Gambo
……………………………………..
Julieth Laizer ,Arusha
Arusha.Wajasiriamali wadogo kutoka nchi za Afrika wamepatiwa elimu ya namna bora ya kufanya biashara kimataifa ili waweze kujikwamua kiuchumi na kukuza biashara zao na hivyo kuweza kupanua wigo wa kufanya biashara kimataifa.
Wajasiriamali hao kutoka nchi za Afrika hii leo wamekutana jijini Arusha kwa lengo la kujadili na kutatua changamoto zinazo wakabili katika soko huru la Afrika .
Akizungumza jijini Arusha katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na shirika la CUTS International ,Mshauri wa sera na biashara kutoka baraza la biashara la Afrika Mashariki (EABC) Adrian Njau amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wajasiriamali hao kujua namna bora za kuboresha biashara zao na kuweza kufanya biashara ndani na nje ya nchi.
Alisema kuwa, mafunzo hayo ya uhalisi wa bidhaa na umuhimu wa kusafirisha bidhaa kutoka Tanzania kwenda nchi za Afrika kwa kutumia soko huru la Afrika na mambo ya viwango ni muhimu kwa wafanyabiashara wanaotaka kupata faida ndani ya soko hilo .
Njau alisema kuwa,uondoaji wa vikwazo kwa wafanyabiashara wadogo ikiwemo kikwazo cha kodi itawasaidia wafanyabiashara kufanya biashara zao kwa ubora na ufanisi ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini Mrisho Gambo alisema kuwa, Serikali inayo fursa ya kumwezesha mfanyabiashara mdogo na kufanikiwa kiuchumi kwa kuweka mazingira rafiki ya ufanyaji wa biashara ndani na nje ya nchi.
Gambo alisema kuwa,kupitia fursa hiyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anaitumia ipasavyo ili waweze kuboresha biashara yake na kuweza kujulikana kimataifa kwa kuongezea bidhaa husika thamani.