Na. Damian Kunambi, Njombe
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa Sunday Deogratias ameliomba baraza la madiwani kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha mbolea za ruzuku zinauzwa kwa bei na utaratibu uliowekwa na serikali badala ya mawakala kuhujumu mbolea hizo na kuuza kwa bei wanazoaka wao.
Hayo ameyasema katika kikao cha baraza la madiwani cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 na kuongeza kuwa kumekuwa na udanganyifu kwa baadhi ya mawakala ambao hutoa nembo za ruzuku na kuziuza kwa utarattibu usio rasmi.
“Waheshimiwa madiwani kuna baadhi ya mawakala ambao tumewabaini wakiuza mbolea kwa utaratibu usio rasmi na tayari mawakala hao wameshaanza kuchukuliwa hatua za kisheria kwani haiwezekani serikali yetu inajitahidi kuwakomboa wananchi juu ya gharama za mbolea halafu wengine wanauza kwa manufaa yao binafsi”. Amesema Deogratias.
Aidha kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri Wise Mgina amesema hakuna sababu ya kuwafumbia macho mawakala wa aina hiyo kwani kwa kufanya hivyo ni kurudisha nyuma juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan na kuwaumiza wananchi.
“Mkurugenzi niwapongeze kwa juhudi mnazo zifanya kwa lengo la kuleta maendeleo katika wilaya yetu hivyo niwasihi muendeleze juhudi hizo nasi madiwani tutawaunga mkono”. Amesema Mgina.