Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Kwaya mpya ya walimu inayofahamika kwa jina la Shinyanga Teachers Choir iliyopo Mkoani Shinyanga imezindua rasmi na kutambulisha Albamu ya kwanza yenye nyimbo zinazoigusa jamii, serikali na Taifa kwa ujumla.
Uzinduzi huo umefanyika usiku, siku ya Ijumaa Oktoba 28,2022 katika ukumbi wa Lyakale Garden uliyopo Manispaa ya Shinyanga na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali pamoja na viongozi wa serikali akiwemo Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga mheshimiwa Elias Ramadhan Masumbuko.
Kwaya hiyo ya chama cha walimu CWT Manispaa ya Shinyanga imetambulisha Albamu mpya inayobeba nyimbo tisa (9) na kwamba Albamu inakwenda kwa jina la “Nani kama Mwalimu”.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alitarajiwa kuwa naibu waziri ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia kazi, vijana na ajira Paschal Patrobas Katambi, ambaye amewakilishwa na Afisa elimu taaluma Mkoa wa Shinyanga Bi. Fausta Luoga.
Afisa elimu taaluma Mkoa wa Shinyanga Bi. Fausta Luoga pamoja na mambo mengine amewapongeza wanakwaya kwa ubunifu wao kwa kutunga nyimbo zenye kufikisha ujumbe katika jamii na serikali ambapo amewasihi kuongeza bidii kutokata tamaa ili kufikia malengo waliyojiwekea.
“Mimi niwapongeze sana wale wote walioanzisha wazo hili la kuwa na kwaya ya walimu niwapongeze sana hii haijawahi kutokea Tanzania nzima siyo jambo la masihara ni jambo la ubunifu na mimi niwahakikishia walimu nitalifikisha hili kwa Mheshimiwa kama lilivyo kwaya yetu hii iwe ni kwaya ya mfano sit u kwa Mkoa wetu huu wa Shinyanga iwe mfano kwa Tanzania nzima”. Amesema afisa elimu taaluma Luoga
“Kwahiyo ni jambo jema sana kwa kikundi chetu cha kwaya mmeona ni vyema kutoa elimu kwa njia ya uimbaji mimi niwapongeze sana lakini pia kuungana na serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na mama yetu mpendwa Samia Suluhu Hassan kushirikiana naye katika majukumu ya uelimishaji wa shughuli mbalimbali za kijamii si hilo tu hii kwaya pia tutaitumia kama ni kwaya ya kuhamasisha kwenye shughuli mbalimbali za kimkoa na kitaifa”.
“Nimesikia katika risala yenu mmeelezea changamoto mbalimbali ambazo mnakutana nazo katika zoezi zima la uendeshaji wa hii kwaya hizi changamoto zinaishia leo hatuwezi tukawa ombaomba wakati sisi kazi yetu niya kuelimisha jamii na kazi yetu tunafanya kwa ajili ya maslahi ya Taifa lote lakini pia sisi tusikate tamaa, tusiogope kama umeamua kuisaidia serikali ya mama Samia Suluhu Hassan naomba songa mbele usirudi nyuma wapo watu wataongea sana sisi tusongembele sote tusimame katika nafasi zetu”.amesema Afisa elimu taaluma Luoga
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mheshimiwa Elias Ramadhan Masumbuko amesema Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga itaendelea kushirikiana na chama cha walimu Manispaa ya Shinyanga katika nyanja zote kupitia kwaya hiyo ili kuleta mabadiliko chanya.
Meya Masumbuko naye ametumia nafasi hiyo kukipongeza chama cha walimu CWT Manispaa ya Shinyanga kwa kuzindua albamu ya nyimbo tisa ambayo inayoitwa “NANI KAMA MWALIMU”
Akizungumza Mwenyekiti wa kwaya hiyo ya walimu ambaye pia ni mjumbe wa kamati ya utendaji Taifa akiwakilisha CWT Mkoa wa Shinyanga Mwalimu Grace Kulwa Hangaya amesema tayari nyimbo hizo zote zinapatikana kwenye ofisi za chama cha walimu Mkoa wa Shinyanga kwa mfumo wa Flashi na sidi (CD) na zinapatikana pia katika mtandao wa kijamii YOU TUBE.