MSAJILI wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) Dkt. Daniel Mushi,akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za bodi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 28,2022 jijini Dodoma.
……………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
MSAJILI wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) Dkt. Daniel Mushi,ameeleza kuwa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2022/23 Tanzania imeuza tani 3,256.60 za nyama nje ya nchi zenye thamani ya Dola za marekani milioni 13.
Hayo ameyasema leo Oktoba 28,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali za bodi hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Dkt.Mushi amesema moja ya mikakati ya Bodi hiyo ni kuongeza kiasi cha nyama kinachouzwa nje ya nchi kwa kushirikiana na Viwanda vya Nyama na wafanyabiashara wanaouza nyama nje.
“Kuweka mikakati ya kulinda masoko ya nyama tuliyonayo kwa sasa tunauza nyama Qatar, UAE, Bahrain, Kuwait, Oman, Comoro, Hong Kong, Jordan, Saudi Arabia.
“Mwaka jana tumeuza tani 10,415 yenye thamani ya milioni 42 za kimarekani, robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2022/23 tumeuza tani 3,256.60 za nyama nje ya nchi zenye thamani ya Dola za marekani milioni 13. Lengo ni kuuza tani 16,000 ifikapo 2026”amefafanua
Dkt.Mushi amesema bodi ina jukumu na mkakati wa kuwahamasisha watanzania kula nyama,kwani ulaji wa nyama kwa kiasi kinachotakiwa ndio njia rahisi ya kuondokana na utapia mlo.
Amesema kuwa kuna watu wamekuwa wakisema nyama ni mbaya lakini uzuri au ubaya wa kula nyama unatokana na kiasi cha nyama mtu anachokula na aina ya nyama anayokula.
“Niseme wazi hapa kuna mkanganyiko kidogo kuna watu wamesema nyama ni mbaya lakini suala la nyama kuwa mbaya au nzuri ni suala la kiasi cha nyama unachokula na aina gani ya nyama unakula,”Dkt Mushi
Dkt.Mushi ameongeza kuwa ili mwili wa binadamu upate virutubisho vyote muhimu anatakiwa kwa wiki walau ale kilo moja ya nyama kwani virutubisho vinavyopatikana kwenye nyama nyekundu havipatikani kwenye mimea na kitaalamu mtu anapaswa kula nyama angalau kilo hamsini kwa mwaka.
Aidha amesema kuwa endapo mtu atakula nyama kwa kiwango kinachotakiwa mtu huyo atakua na afya kwani itasaidia kuimarisha kinga ya mwili ya kupambana na magonjwa nyemelezi na kuongeza nguvu ya kufanya kazi hivyo itasaidia kuongeza uzalishaji.
“Kama mnavyo fahamu nyama ndio njia rahisi ya kuondokana na utapia mlo, mtu anapowaambia watanzania wasile nyama nadhani haelewi vizuri hali ilivyo katika ulaji wa nyama na sisi kama Serikali tunao mpango wa kuhamasisha watanzania wale nyama lakini ulaji nyama uliosahihi,”Amesema Dkt.Mushi
Katika hatua nyingine amesema kuwa bodi itahakikisha inalinda afya ya mlaji kupitia udhibiti na ukaguzi sambamba na kuhamasisha uzajishaji bora wa nyama ili kupata masoko nje ya nchi.
Kwasasa mtanzania mmoja anakula nyama takribani kilo 15 kwa mwaka kuanzia Januari mpaka Disemba lakini tunapaswa kula nyama angalau kilo 50 kwa mwaka, kwa wenzetu Ulaya wanakula mpaka kilo 100 mtu mmoja kwa mwaka
“Sasa unapokula nyama kiasi kinachotakiwa kwanza unakuwa na afya unakuwa na nguvu ya kufanya kazi na uzalishaji unaongezeka lakini pia unakuwa na uwezo wa kinga ya mwili kuweza kujikinga na magonjwa kinga zinakuwa imara,”Ameeleza Dkt.Mushi