Naibu Katibu Mkuu wa Waziri wa Maliasili na Utalii, Juma S. Mkomi akizungumza leo Jijini Dodoma wakati wa kikao na Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakati wa uwasilishaji wa semina fupi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Idara ya Malikale
Mjumbe wa wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii ambaye pia ni mbunge w Viti Maalum wa Tabora, Mhe. Haw Mwaifunga akitoa mchango wake wa kuboresha rasilimali za Malikale mara baada ya uwasilishaji wa semina fupi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Idara ya Malikale
Mkurugenzi wa Idara ya Malikale akitoa ufafanuzi leo Jijini Dodoma mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii mara baada ya kuwasilisha wa semina fupi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Idara ya Malikale
Baadhi ya Watendaji kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii wakifuatilia michango ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii mara baada ya uwasilishaji wa semina fupi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Idara ya Malikale
****************
Naibu Katibu wa Maliasili na Utalii, Juma S. Mkomi ametoa wito kwa Wabunge kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuyalinda na kuyatunza maeneo ya Malikale kwani ni rasilimali isiyorejesheka pale inapoharibiwa.
Ametoa kauli hiyo leo Jijini Dodoma mara baada ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupata semina fupi kuhusu utekelezaji wa majukumu wa Idara ya Mambo ya Kale iliyotolewa na Mkurugenzi wa Idara hiyo Dkt. Christowaja Ntandu.
Naibu Katibu Mkuu Juma Mkomi amesema Malikale ni rasilimali ambayo ikiharibiwa inapoteza thamani yake, iko tofauti na wanyamapori ambao kama ikitokea wametoweka hapa nchini juhudi za kuwarejesha zinaweza kufanyika wakasafirishwa kutoka katika nchi nyingine kwa ajili ya kuendeleza kizazi
‘Rasimali ya Malikale ni urithi wa Taifa sio kama wanyamapori kama faru au tembo kuwa wakipotea hapa nchini tunaweza tukaomba kwa nchi jirani watugawie tukawatunza wakazaliana, kwenye Malikale hili suala halipo’’ amefafanua Mkomi
Kufuatia hali hiyo, Mkomi ametoa wito kwa Wadau wote hapa nchini wakiwemo Wabunge ambao ni Madiwani katika vikao vya Halmashauri kuendelea kushirikiana na Wizara katika kuuthami Malikale zilizopo hapa nchini kwa ajili ya faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Katika hatua nyingine, Mkomi amewaomba Wabunge hao wawe Mabalozi katika maeneo yao kwa kuwa katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la uharibifu na uvamizi wa maeneo ya Malikale ambayo yamekuwa yakipangiwa matumizi mengine hali inayoathiri historia ya Taifa.
”Sisi kama Wizara yenye dhamana hatufurahii jambo hili na kwa sasa Halmashauri zote ambazo zimebadalisha matumizi ya meneo ya malikale tumeanza kuwasiliana nazo ili maeneo husika yaachwe na kuheshimiwa kama maeneo yenye kumbukumbu muhimu kwa taifa letu” amesisitiza Mkomi
Ameongeza kuwa Malikale ni sekta muhimu inayochangia katika uhifadhi wa urithi wa Taifa, mazingira, maendeleo ya kiuchumi, kiutamaduni na kijamii huku akitoa mfano wa nchi kama Misri imekuwa ikipokea maelfu ya watalii kuja kutembelea maeneo ya malikale
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Juma Ally Makoa amesema Malikale ni uchumi hivyo ni wajibu wa kila Mbunge katika eneo lake kulisemea jambo hilo ” Wenzetu huko nje wanapata fedha nyingi sana kutokana na watalii kupitia aina hii ya utalii” amesema Mhe. Makoa
Mhe. Makoa ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii ihamasishe jamii kuanzisha Makumbusho za Jamii kama vile Wa-iraqw kwa lengo la kuenzi na kutunza tamaduni zao.
Pia amesisitiza matumizi zaidi ya digitali katika kutunza na kulinda rasilimali za malikale ili kuteka soko la vijana ambao kwa sasa ndiyo watumiaji wakubwa wa mifumo hiyo ya Kidigitali .