Tanzania inakuwa nchi ya kwanza katika Bara la Afrika na ya 12 duniani kuwa mwenyeji Mashindano ya Dunia ya Urembo, Utanashati na Mitindo kwa Viziwi Duniani baada ya mashindano hayo kufanyika mara 12 baada ya kuanzishwa kwake.
Kauli hiyo imetolewa katika mkutano wa Waandishi wa Habari leo Oktoba 28,2022 jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbas na Rais wa Mashindano ya Urembo na Utanashati kwa Viziwi Duniani, Bonita Lee kutoka nchini Marekani.
Shindano hilo litafanyika kesho JNICC Dar ea Salaam ambapo Mhe Rais Samia Suluhu Hassan atawakilishwa na Mhe. Doroth Gwajima Waziri wa Jinsia, Wanawake na Makundi maalum Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye atakuwa mgeni maalum.
Dkt. Abbas amefafanua kuwa Serikali imewapa zawadi washindi wote wa shindano hilo la kidunia na viongozi kutembelea mbuga ya Wanyama ya Ngorongoro Oktoba 31,2022 baada ya kumalizika kwa shindano hilo kesho ikiwa ni mwendelezo wa Royal Tour aliyoiasisi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
Amesema tukio hilo litarushwa na mitandao mbalimbali duniani ikiwa na pamoja na kituo cha televisheni cha AZAM ambacho kitarusha mbashara kupitia kipindi chake cha Sinema zet kuanzia majira ya saa mbili usiku.
Pia amesema katika tukio hili maalum itawajumuisha waalikwa zaidi ya 1000 ambapo filamu ya Royal Tour iliyochezwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan itaanza kuonyeshwa ili watu waweze jinsi Tanzania ilivyobarikiwa kuwa na vivutio mbalimbali vya utalii.
Aidha, ameongeza kwamba burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii wa miziki mbalimbali zitaoneshwa kwa washiriki na ameomba washiriki kuwa tayari kupokea matokeo kutoka kwa majaji kwani hadi kufika hapa tayari wote ni washindi.