Na. Zillipa Joseph, Katavi
Kati ya watoto 10 hadi 15 wanalazwa kwa mwezi katika kituo cha afya cha Katumba katika Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi kwa sababu ya utapiamlo mkali huku watoto wengine kati ya 30 hadi 40 wanatibiwa na kuruhusiwa kutokana na tatizo hilo la utapiamlo.
Akitoa taarifa mganga mfawidhi wa kituo hicho cha afya Dk. Venanda Msati amesema kwa watoto wenye utapiamlo wa kawaida wanapatiwa chakula dawa na kuwaelimisha wazazi namna ya kuwaandalia chakula watoto wao ili waweze kuwa na hali nzuri
Aidha kwa watoto wenye utapiamlo mkali wanalazwa na kupatiwa chakula dawa mpaka watakapopata nafuu na baadaye wanaruhusiwa kutoka hospitali.
Dk. Msati amesema chanzo kikuu cha utapiamlo ni wazazi kutingwa na kazi nyingi na hivyo kushindwa kuwa uangalizi mzuri wa watoto wao.
Chakula kipo lakini tatizo kubwa hapa ni wazazi kutokuwa na elimu ya makuzi ya watoto na badala yake wamekuwa wakiwaacha kwa muda mrefu na watoto wenzao hali inayopelekea kushindwa kupatiwa chakula sahihi’ alisema
Aliongeza kuwa chanzo kingine cha utapiamlo ni watoto waliougua kwa muda mrefu huku wengine waliopoteza wazazi kushindwa kupata uangalizi mzuri hali inayopelekea utapiamlo.
Bi. Veronica Mbaula ni mkazi wa Mnyaki katika kata ya Katumba amekiri kuwa yeye ana mjukuu mwenye utapiamlo, na kuongeza kuwa chanzo kikubwa ni umaskini kwani wanamtegemea mtoto wake akafanye vibarua ndipo wapate chakula ambapo kuna siku wanakula mara moja au mbili kwa kutwa nzima kutokana na chakula watakachokuwa nacho siku hiyo.
Aidha wakazi wengine wa katumba wanadai kuwa walikuwa walikima katika mashamba ambayo walinyang’anywa na serikali kutokana na ukweli kwamba yapo ndani ya hifadhi na hivyo kubadilisha maisha yao na kuwa magumu hali inayopelekea wakati mwingine kulala njaa.