Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya Ulaya Bi. Jutta Urpilainen, baadaa ya kuzindua mpango wa pili wa msaada wa Umoja wa Ulaya kwa Tanzania wenye thamani ya euro milioni 166 sawa na shilingi bilioni 380 kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiteta jambo na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya Ulaya Bi. Jutta Urpilainen, baadaa ya kuzindua mpango wa pili wa msaada wa Umoja wa Ulaya kwa Tanzania wenye thamani ya euro milioni 166 sawa na shilingi bilioni 380 kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akizungumza na waandishi wa vyombo vya habari mbalimbali nchini wakati wa mkutano pamoja na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya Ulaya Bi. Jutta Urpilainen, (hayupo pichani), wakati wakitangaza mpango wa pili wa msaada wa Umoja wa Ulaya kwa Tanzania wenye thamani ya euro milioni 166 sawa na shilingi bilioni 380 kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, Jijini Dar es Salaam.
Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya Ulaya Bi. Jutta Urpilainen akifafanua jambo wakati wa kikao na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (hayupo pichani) jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Mhe. Manifredo Fanti.
Mkutano ukiendelea, ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya Ulaya Bi. Jutta Urpilainen, jijini Dar es Salaam, kabla ya kuzindua mpango wa pili wa msaada wa Umoja wa Ulaya kwa Tanzania wenye thamani ya euro milioni 166 sawa na shilingi bilioni 380 kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (katikati) na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya Ulaya Bi. Jutta Urpilainen (wan ne kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi kutoka Tanzania na baadhi ya viongozi kutoka Umoja wa Ulaya, baadaa ya kuzindua mpango wa pili wa msaada wa Umoja wa Ulaya kwa Tanzania wenye thamani ya euro milioni 166 sawa na shilingi bilioni 380 kwa ajili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, Jijini Dar es Salaam jijini Dar es Salaam.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-WFM, Dar es Salaam)
**********************
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Umoja wa Ulaya (EU) umeipatia Tanzania msaada wa euro milioni 166 sawa na takribani shilingi za Tanzania bilioni 380 ajili ya utekelezaji wa miradi mitatu ikiwemo kuibua fursa zitokanazo na bahari (uchumi wa buluu), sekta Jumuishi ya fedha na kuimarisha ushirikiano.
Msaada huo umetangazwa leo tarehe 26 Oktoba, 2022 Jijini Dar es Salaam mbele ya wanahabari na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya Ulaya Mhe. Jutta Urpilainen na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.
Dkt. Nchemba alisema kuwa msaada huo umeidhinishwa na Umoja wa Ulaya katika mwaka wa pili wa utekelezaji wa ushirikiano kati ya Tanzania na Umoja wa Ulaya kwa kipindi cha miaka saba kuanzia mwaka 2021 hadi 2027, ambapo katika awamu ya kwanza, tarehe 22 Machi, 2022, Serikali ilipokea msaada wa euro milioni 180, sawa na zaidi ya shilingi za Tanzania bilioni 400.
Alifafanua kuwa katika awamu hiyo ya pili ya msaada wa euro milioni 166, mradi wa uchumi wa buluu umetengewa euro milioni 110, mradiwa kuimarisha sekta ya fedha (euro milioni 50) na mradi wa kuimarisha ushirikiano umetengewa euro milioni 6.
“Fedha hizi ni sehemu ya matokeo ya ziara ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, iliyofanyika mwezi Februari, 2022 jijini Brussels, nchini Ubelgiji ambapo Umoja huo ulitangaza kuipatia Tanzania msaada wa kiasi cha euro milioni 426 kwa kipindi cha miaka minne ijayo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini” alisema Dkt. Nchemba
Dkt. Nchemba aliushukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada huo mkubwa ambao ameahidi kuwa miradi itakayonufaika na fedha hizo itatekelezwa kwa viwango na kama ilivyokusudiwa kwa ajili ya kuwaletea wananchi maendeleo kwa haraka.
Alisema Tanzania inathamini kwa kiwango kikubwa ushirikiano uliopo kati yake na Umoja wa Ulaya tangu uanzishwe mwaka 1975 ambapo hadi sasa Umoja huo umetoa misaada na mikopo yenye thamani ya euro bilioni 2.4 sawa na takribani shilingi trilioni 5.9 na mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya euro milioni 270.9 sawa na shilingi bilioni 706.5.
Kwa upande wake, Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya Ulaya, Mhe. Jutta Urpilainen, alisema Tanzania ni mshirika muhimu wa Umoja wa Ulaya ikiwa ni nguzo imara inayounganisha Mashariki na Kusini mwa Afrika na na kuipongeza kwa kujiimarisha katika nafasi ya uchumi wa kati.
kuwa Umoja huo unafurahishwa na maendeleo makubwa ya kiuchumi yaliyofikiwa nchini na kwamba wako tayari kuendelea kutoa misaada ili kufanikisha agenda hiyo.
Alisema kuwa msaada huo wa euro milioni 166 umelenga kuimarisha shughuli za uchumi wa buluu uliolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuvumbua fursa za kiuchumi zinazopatikana kupitia bahari ili taifa na jamii inayozunguka fukwe za bahari iweze kunufaika kupitia uvuvi, utalii wa kiikolojia, huku ikihifadhi mazingira na kukuza ajira.
Alisema manufaa mengine ya mpango huo ni kuiwezesha jamii kuzifikia fursa za kiuchumi kupitia taasisi za fedha, uwekezaji wenye lengo la kuchochea mapinduzi ya kilimo, uchumi jumuishi na maendeleo endelevu nchini Tanzania, kuboresha ujuzi wa wananchi na kuboresha mazingira ya sheria mbalimbali.
“Msaada huo umelenga kutekeleza mkakati wa Umoja wa Ulaya ujulikanao kama The Global getway, wenye lengo la kuboresha mifumo ya kidijitali, mabadiliko ya tabianchi, afya, elimu, miundombinu ya usafiri na masuala ya utafiti kwa kuzishirikisha sekta ya umma na sekta binafsi nchini Tanzania” alisema Mhe. Urpilainen
“Watekelezaji wa miradi hii watafanyakazi bega kwa bega na Serikali kutekeleza malengo hayo kwa kutumia misaada ya fedha kutoka Umoja wa Ulaya ili kuongeza uwekezaji zaidi hapa nchini” aliongeza Mhe. Urpilainen.
Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa wa Kamisheni ya Ulaya, Mhe. Jutta Urpilainen, yuko nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili na baadae ataelekea nchini Malawi kwa ziara kama hiyo.