Mwenyekiti wa bodi ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini,Mwantum Mahiza akizungumza na waandishi wa habari katika kikao hicho cha wadau jijini Arusha leo.
Kaimu msajili wa NGO’s nchini ,Mussa Sang’anya akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kikao hicho Leo jijini Arusha.
Mkurugenzi wa shirika la kutoa malezi kwa watoto SOS Tanzania,David Mulongo akizungumza kwenye kikao hicho cha wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya utetezi kwa watoto kilichofanyika jijini Arusha.
………………………….
Julieth Laizer ,Arusha.
Matukio ya ukatili wa kijinsia kwa watoto yanaendelea kushika kasi kutokana na wazazi wengi kutokuwa na muda na watoto hali inayowafanya watoto kujiingiza kwenda mambo yasiyofaa na kufanyiwa ukatili zaidi.
Aidha hali ya ukatili wa watoto kwa sasa hivi inaelezwa kuwa mbaya na hiyo ikichangiwa na wazazi wenyewe kutokuwa na muda na watoto hivyo watoto kukosa elimu ya makuzi yaliyobora na hivyo kupeleka kufanyiwa ukatili .
Hayo yalisemwa Leo jijini Arusha na Mwenyekiti wa bodi ya mashirika yasiyo ya kiserikali nchini ,Mwantum Mahiza wakati akizungumza katika kikao maalumu cha wadau wanaojihusisha na masuala ya watoto jijini Arusha .
Mahiza amesema kuwa, kwa sasa hivi watoto wetu hawapo salama kwani wanafanyiwa mambo ya ajabu na ya kutisha na wanaofanya hivyo ni ndugu wa karibu jambo ambalo linawafanya watoto wakose amani hata ya kukaa kwenye familia zao.
Amesema kuwa,watoto wanafanyiwa ukatili kwa kiwango kikubwa sana hivyo ni jukumu la wadau mbalimbali wanaojihusisha na maswala ya watoto kuhakikisha kila mmoja kwa nafasi yake anawajibika kutoa elimu kwa jamii kuhusu makuzi na malezi na swala zima la maadili.
” mifumo iliyopo kuanzia ngazi za chini ikitumika vizuri itasaidia kuzuia maswala ya ukatili wa kijinsia wanaofanyiwa watoto kwani huko ndiko sehemu sahihi watoto wataweza kuripoti matukio wanayofanyiwa kwa urahisi zaidi na kuweza kuchukuliwa hatua za kisheria mapema .”amesema Mahiza.
Aidha ametaka swala zima la ukatili wa kijinsia kwa watoto kushirikishwa wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa mila,viongozi wa dini katika ngazi zote ili kwa pamoja waweze kuongeza nguvu kukemea na kudhibiti matukio hayo kwani hali ya watoto kwa sasa ni mbaya na ukatili umekuwa mkubwa sana.
Kwa upande wa Kaimu Msajili wa mashirika yasiyo ya kiserikali nchini (NGO’S) ,Mussa Sang’anya amesema kuwa,swala zima la ukatili wa kijinsia kwa watoto bado ni changamoto kubwa sana, hivyo nguvu zaidi inatakiwa kuongezwa kwa mashirika na hata wadau mbalimbali ili kwa pamoja kuweza kushirikiana katika kukemea matukio hayo.
“Leo tumekutana hapa na ni kikao kazi cha pamoja kuhakikisha kila mmoja wetu anakuja na maazimio na mikakati ya kufanya katika kudhibiti swala zima la ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto wetu na sisi kama wizara tutaendelea kutoa miongozo mbalimbali kuhakikisha watoto wanakuwa salama kila wakati.”amesema .
Aidha ameyataka mashirika binafsi yanayotetea haki za watoto kuwa na nia moja ya dhati katika kusaidia watoto kupata haki zao na kuhakikisha usalama wa mtoto unaendelea kulindwa ,na kuhakikisha rasilimali zinazopatikana kwa ajili ya watoto zinasambaa nchi nzima ili wote wapate huduma .
Naye Mkurugenzi wa shirika la kutoa malezi kwa watoto SOS Tanzania,David Mulongo amesema kuwa wao kama shirika wamekuwa wakifanya maswala ya kutetea na kuelimisha jamii kuhusu haki za watoto kwani swala la kusaidia watoto ni la kila mmoja wetu kuhakikisha wote kwa pamoja wanashirikiana kutokomeza ukatili wa kijinsia ambao wamekuwa wakifanyiwa watoto kwa kiwango kikubwa.
“Kikao hiki kimeandaliwa na wizara kwa kushirikiana na sisi shirika katika kuangalia namna ya kuweka mikakati itakayosaidia kuwaokoa watoto hawa kwani watoto wapo katika hatari kubwa kutokana na ukatili wanaofanyiwa kuanzia majumbani,kwenye taasisi wanazopata huduma hali ambayo imesababisha kuwepo kwa ongezeko kubwa la watoto wa mitaani.”amesema Mulongo.
Ameongeza kuwa,nchi yetu ina sera nzuri na mfumo mzuri wa kiutawala pamoja na sheria nzuri ila changamoto ni kwamba lazima wadau waangalie wajue katika nafasi waliyopewa wajengewe mazingira ya kuona swala la kulinda haki ya watoto liwe ni wajibu wa kila mmoja katika serikali jamii na hata asasi za kidini na kuna haja ya kuwepo kampeni ya kitaifa kuhakikisha kila mdau anajengewa uwezo kama kukumbushwa wajibu kuwa swala la kumlinda mtoto ni wajibu wa kila mmoja.